UN: Imarati inasaidia magenge ya watu wenye silaha magharibi mwa Sudan
(last modified Sun, 06 Feb 2022 04:41:17 GMT )
Feb 06, 2022 04:41 UTC
  • UN: Imarati inasaidia magenge ya watu wenye silaha magharibi mwa Sudan

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti yake maalumu na kusema kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu unayasadia magenge yenye silaha katika jimboi la Darfur la magharibi mwa Sudan.

Katika ripoti yake hiyo ya kila mwaka, Umoja wa Mataifa umesema pia kuwa, mamluki wanaodhaminiwa kifedha na Imarati nchini Libya ndicho chanzo kikuu cha kifedha za magenge mengi yenye silaha kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan.

Katika ripoti yao hiyo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, awali misaada ya kifedha ya Umoja wa Falme za Kiarabu ilikuwa inatumwa kwa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar. Hivi sasa Imarati inalitumia kundi hilo kuyafikishia fedha magenge yenye silaha ya magharibi mwa Sudan.

Jenerali muasi, Khalifa Haftar

 

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ambayo imeandaliwa na wataalamu wa kitengo cha kusimamia utekelezaji wa marufuku ya silaha kwa makundi ya Sudan imeongeza kuwa, migogoro nchini Sudan  na hasa katika jimbo la Darfur itaendelea kuweko kutokana na kutoheshimiwa marufuku ya kutumiwa silaha magenge ya waasi ya maeneo hayo.

Tangu mwaka 2003 jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan limekumbwa na mapigano baina ya waasi na askari wa serikali na baina ya makundi ya waasi wao kwa wao.

Inakadiriwa kuwa karibu watu laki tatu wameshauwa na milioni mbili na laki tano wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mgogoro wa jimbo hilo tangu mwaka 2003 hadi hivi sasa.

Tags