Mahmoud Abbas asisitiza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8008-mahmoud_abbas_asisitiza_kuundwa_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_palestina
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametaka kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itafanya kazi kulingana na ratiba na mipango ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2016 23:43 UTC
  • Mahmoud Abbas asisitiza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Palestina

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametaka kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itafanya kazi kulingana na ratiba na mipango ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO).

Mahmoud Abbas, ametoa wito huo katika kikao cha dharura cha baraza la mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilichofanyika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Cairo, Misri.

Mbali na kusisitiza juu ya kuundwa serikali hiyo itakayoshirikisha Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), Abbas amesema serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina inapaswa itekeleze siasa na sera za PLO kwa sababu serikali ya Mamlaka ya Ndani pia inafanya kazi kwa kufuata sera hizo.

Akiashiria msimamo wa Hamas wa kutangaza kuwa iko tayari kwa uchaguzi, Mahmoud Abbas amesema, mwaka 2006 ulifanyika uchaguzi, na hivi sasa baada ya miaka 10 inapasa ufanyike uchaguzi wa kumchagua Rais wa Mamlaka ya Ndani na Bunge ili kambi ya ndani ya Palestina iwe kitu kimoja na iliyoungana.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza pia kuwa kwa irada ya nchi za Kiarabu na Jamii ya Kimataifa inapasa yaandaliwe mazingira ya kuhakikisha taifa la Palestina linakuwa huru na kupatikana njia ya ufumbuzi wa kiadilifu kuhusu suala la wakimbizi na kuundwa nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967.../