Mazungumzo baina ya Iran na Oman kuhusu usalama wa baharini
(last modified Thu, 10 Mar 2022 04:10:03 GMT )
Mar 10, 2022 04:10 UTC
  • Mazungumzo baina ya Iran na Oman kuhusu usalama wa baharini

Kikao cha Tatu cha Makamanda wa Gadi ya Ufukweni ya Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran na Oman kimefanyika mjini Muscat na kujadili usalama wa baharini. Maudhui kuu iliyojadiliwa na nchi hizi mbili ndugu katika kikao hicho ni kuzidi kushirikiana na kuwa na uratibu wa pamoja na kulinda usalama wa mpaka wa baharini wa nchi hizo.

Ali Bin Seif al-Muqbeli, Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Ufukweni cha Oman ndiye aliyeongoza timu ya nchi hiyo katika mazungumzo huku timu ya Iran ikiongozwa na Hassan Kargar, Naibu Kamanda wa Gadi ya Ufukweni ya Iran. Kila mwaka vikosi vya baharini vya Iran na Oman na majeshi ya polisi na gadi za fukweni, huwa zinafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwa ajili ya kulinda usalama wa mipaka ya baharini ya nchi hizo mbili. Mwaka 2019, wakati jopo la kijeshi la Iran lilipotembelea Oman, nchi hizi mbili zilitiliana saini hati maalumu ya maelewano.

Oman ni nchi ambayo ina uhusiano wa jadi na mzuri na Iran tangu kale. Hata kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, uhusino wa Tehran na Muscat ulikuwa mzuri. Licha ya kuweko mivutano na migogoro mingi katika eneo la Ghuba ya Uajemi, na licha ya Marekani kufanya njama za kila namna za kueneza chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini muda wote uhusiano wa Oman na Iran haujawahi kuharibika na wakati wote nchi hizi mbili zimeendelea kuchunga msingi wa kuheshimiana na kuzingatia maslahi ya pamoja. Viongozi wa Oman wanaamini kuwa, uhusiano wao wa karibu na Iran umesimama juu ya msingi wa kuangalia uhalisia wa mambo na kwamba Iran ni jirani muhimu sana kwa Oman. Nchi hizi mbili hazina hitilafu zozote za mpakani. Uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Oman katika masuala tofauti umekuwepo muda wote na katika mazingira yote. 

Nchi mbili za Iran na Oman zina uhusiano mzuri na wa kidugu katika nyuga tofauti

 

Mir Javad Mirgoli Bayat, mtaalamu wa masuala ya eneo la Asia Magharibi anasema, Iran na Oman zinaelewana sana na zinatambua wasiwasi na daghadagha ya kila mmoja wao katika masuala tofauti. Uhusiano wa nchi hizi mbili umevuka hatua ya kuishi pamoja kwa salama na umeingia kwenye daraja ya juu zaidi ya ustawishaji wa pande zote wa uhusiano wao wa kiuchumi na kiusalama na hivi sasa unaelekea upande wa kuwa washirika wanaoaminiana sana. 

Katika kipindi cha miaka yote hii, nchi hizi mbili zimefanya juhudi za kila namna za kuimarisha na kutia nguvu uhusiano wao. Miongoni mwa kazi zilizofanywa katika uwanja huo ni kuuundwa kamati tofauti za pamoja za kiistratijia, kisiasa, kijeshi, kiufundi, kiushirikiano, kielimu na ulinzi wa pamoja wa fukwe za baharini. Kiujumla kati ya nchi za eneo hili, Iran na Oman zina uhusiano bora kabisa na ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine kieneo na kimataifa. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Oman

 

Uhusiano wa kiulinzi na kijeshi wa Iran na Oman mbali na ushirikiano mwingine mwingi, una umuhimu mkubwa na wa kipekee na muda wote umekuwa ukishika nafasi ya kwanza katika uhusiano wa mataifa haya mawili ndugu ya Waislamu. Nchi hizi mbili zina ushirikiano mzuri sana katika ulinzi wa baharini na Oman ni mshirika wa kiistratijia wa Iran katika kulinda usalama wa Lango Bahari la Hormuz. Naam, kulindwa usalama wa Lango Bahari la Hormuz katika pande zote za kisiasa, kiuchumi na kiusalama ni muhimu sana kwa Jamhuri ya Kiislamu na Oman.

Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja Oman kuwa ni nchi rafiki na ndugu. Amesisitiza kuwa, nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi ya Oman ni kubwa na kila mtu anaiona duniani kutokana na nchi hizi mbili kuangaliana moja kwa moja na Lango Bahari la Hormuz. Kupenda amani na urafiki ni katika misimamo muhimu sana na ya kimsingi ya nchi hizi mbili. Licha ya kuweko njama za kila namna za maadui za kujaribu kuharibu uhusiano wa Iran na Oman, lakini uhusiano wa mataifa haya mawili ndugu ya Waislamu unaendelea kuimarika na kustawi zaidi na zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele.

Tags