Ansarullah: Operesheni ya Bnei Brak huko Palestina imewatikisa Wazayuni
Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen ilitoa taarifa jana Jumatano ikipongeza operesheni ya mwanamapambano wa Palestina huko Bnei Brak, Mashariki mwa Tel Aviv na kusema kuwa, operesheni hiyo imetikisa nguzo za utawala ghasibu wa Israel.
Jumanne iliyopita eneo hilo la "Bnei Brak" lilishuhudia operesheni ya kijasirii iliyofanywa na mwanamapambano wa Palestina, Zia Hamarsheh, ambaye aliuawa shahidi. Wazayuni 5 waliuawa na wengine 6 walijeruhiwa katika operesheni.
Taarifa hiyo ya harakati ya Ansarullah ya Yemen imesisitiza kuwa, operesheni hiyo ya mwanajihadi na operesheni nyingine za hivi karibuni zinathibitisha kwamba, ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu hazitakuwa salama kamwe kwa wavamizi hao, na kwamba njia ya mapambano na jihadi bado inaendelea kustawi.
Taarifa hiyo imewapongeza Mujahidina wa Palestina, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kusisitiza kwamba, msimamo thabiti wa Ansarullah wa kuunga mkono matakwa na mapambano ya wananchi wa Palestina bado uko imara.
Kabla ya hapo makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina yalikuwa tayari yamekaribisha operesheni hiyo ya muqawama na kutangaza kuwa ni jibu kwa ukatili wa Wazayuni maghasibu. Makundi hayo yamesema operesheni dhidi ya Wazayuni ya wananchi wa Palestina itaendelea maadamu wavamizi hao wanaendelea kufanya jinai na uhalifu dhidi ya wananchi wa Palestina.
Wakati huo huo Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah imeeleza upinzani wake kamili dhidi ya mkutano wa Naqab na kuutaja kuwa ni mkutano wa usaliti. Imeeleza kuwa mkutano huo ulifanyika kwa lengo la kula njama dhidi ya mataifa ya Kiislamu na matukufu ya dini hiyo.
Siku ya Jumapili iliyopita mawaziri wa mambo ya nje wa nchi nne za Kiarabu za Misri, Imarati, Bahrain na Morocco walishiriki katika mkutano maalumu uliohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Utawala wa Kizayuni, Yair Lapid na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu la Naqab.
Inasemekana kuwa suala la Iran, mgogoro wa Ukraine na kuhalalisha uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika kikao hicho.