Bunge la Pakistan lazuia kuuzuliwa Imran Khan, lakosoa uingiliaji wa maajinabi
(last modified Mon, 04 Apr 2022 02:35:19 GMT )
Apr 04, 2022 02:35 UTC
  • Bunge la Pakistan lazuia kuuzuliwa Imran Khan, lakosoa uingiliaji wa maajinabi

Bunge la Pakistan limetupilia mbali mpango wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Imran Khan, likieleza kuwa limechukua hatua hiyo kutokana na uingiliaji wa madola ya kigeni kwenye mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Qasim Khan Suri, Naibu Spika wa Bunge la Taifa la Pakistan jana Jumapili alitupa nje hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Imran Khan akisisitiza kuwa, mpango huo unaenda kinyume na Sura ya 5 ya Katiba ya nchi hiyo.

Ameeleza bayana kuwa, hakuna dola lolote ajinabi litaruhusiwa kuiondoa madarakani serikali halali iliyochaguliwa na wananchi, kupitia njama za maajinabi.

Baadaye hiyo jana, Rais wa Pakistan, Arif Alvi alilivunja Bunge hilo kutokana na ushauri aliopewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Imran Khan.  Kuvunjwa Bunge la Pakistan kunamaanisha kuwa, nchi hiyo italazimika kufanya uchaguzi katika kipindi cha siku 90 zijazo.

Khan alikuwa ametoa wito wa maandamano Jumapili kabla ya kupigwa kura ya kutokuwa na imani naye

Imran Khan kwa upande wake anasisitiza kuwa, harakati za kutaka kumuondoa madarakani ni uingiliaji wa wazi wa Marekani katika siasa za ndani za Pakistan na kwamba ni jaribio la "kubadilisha utawala."

Khan anaamini kuwa, mashinikizo ya vyama vya upinzani yanayomtaka ajiuzulu yanatokana na njama za nchi za kigeni kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali yake kutokana msimamo wake usioyumba kuhusu siasa zake za nje na ndani ya nchi.