Upinzani Bahrain wataka kutimuliwa nchini humo vikosi vya jeshi la Marekani
(last modified Thu, 07 Apr 2022 01:57:16 GMT )
Apr 07, 2022 01:57 UTC
  • Upinzani Bahrain wataka kutimuliwa nchini humo vikosi vya jeshi la Marekani

Kundi moja la upinzani nchini Bahrain limelaani uwepo wa vikosi vya majini vya Marekani nchini humo na kusisitiza kuwa, wakati umefika wa kufunga kambi ya kijeshi na kuwafukuza wanajeshi wa US katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.

Mrengo wa Vijana wa Harakati ya Februari 14 umesema katika taarifa kuwa: Moja ya malengo makuu ya uwepo wa kambi ya kijeshi ya Marekani nchini humo ni kuupa himaya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa, ambao nao unahudumia maslahi ya Washington nchini Bahrain.

Mrengo huo wa upinzani umeeleza kuwa, kituo cha kijeshi cha Marekani nchini Bahrain kimewapa mafunzo mamluki wa Jordan, Pakistan, Yemen na Syria, juu ya namna ya kukandamiza harakati ya mwamkoa ya Februari 14 nchini humo.

Tarehe 14 Februari mwaka huu, ilisadifiana na mwaka wa 11 wa mwamko na mapambano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kidikteta na kiukoo wa Aal Khalifa.

Wanachama wa Mrengo wa Vijana wa Harakati ya Februari 14

Mrengo wa Vijana wa Harakati ya Februari 14 umeeleza katika taarifa yake kuwa, tangu serikali ya Manama ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel Septemba 2020, Bahrain imegeuzwa pango la ujasusi, na kituo kikuu cha kuendeshea harakati za kijasusi dhidi ya Iran na makundi ya muqawama katika eneo.

Harakati hiyo ya upinzani nchini Bahrain imetaka kufungwa mara moja kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko Juffair, yapata kilomita 8 kusini mashariki mwa Manama, mji mkuu wa nchi hiyo, sambamba na kutimuliwa nchini humo wanajeshi na washauri wa kijeshi na kiusalama wa Marekani na utawala haramu wa Israel.