Radiamali ya Iran kufuatia kuongezewa adhabu ya kifungo Sheikh Ali Salman
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hatua ya kumzidishia adhabu ya kifungo cha jela Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al Wifaq ya Bahrain.
Sadeqi Hussein Jaberi Ansari, amesema amesikitishwa na kuidhinishwa na kuongezewa kifungo cha jela Sheikh Ali Salman na kueleza kuwa, hatua za aina hiyo dhidi ya viongozi wa kisiasa wenye misimamo ya wastani si suluhisho la matatizo ya Bahrain.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa kushadidishwa hatua dhidi ya viongozi wa kisiasa na kimapinduzi wa Bahrain na kuyafanya matatizo ya nchi hiyo kuwa tata, yote hayo mwishowe yatakuwa ni kwa maslahi ya pande zenye misimamo mikali.
Mahakama ya Rufaa ya Bahrain juzi ilizidisha hukumu ya kifungo cha jela cha miaka minne aliyokuwa amekatiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al Wifaq ya Bahrain hadi miaka tisa. Jumuiya ya Kiislamu ya Kitaifa ya al Wifaq ya Bahrain imeitaja hukumu hiyo iliyotolewa kwa Katibu wake Mkuu kuwa ni ya kichochezi na iliyoshindwa na kwamba hukumu hiyo itaendeleza tu mgogoro wa kisiasa nchini Bahrain.