Sana'a: Umoja wa Mataifa unataka kupora haki za Wayemen
Mjumbe wa timu ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa yenye makao makuu yake Sana'a, mji mkuu wa Yemen amesema kuwa, hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kulitambua baraza la uongozi wa Yemen lililoundwa na Wasaudia, ni kupora haki za wananchi wa Yemen.
Alquds al Arabi imemnukuu Abdul Malik al Ajri akisema hayo leo kujibu uamuzi huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, si jambo la kushangaza kuuona umoja huo ukifurahishwa na hatua ya ukoo wa Aal Saud ya kuunda baraza jipya la uongozi baada ya kumvua madaraka kibaraka wake mwingine Abdu Rabbuh Mansur Hadi kwani Umoja wa Mataifa umethibitisha kivitendo katika kipindi chote cha vita vya kivamizi huko Yemen kwamba uko tayari kupokea na kukubali hatua yoyote inayochukuliwa na Saudia.
Wiki moja iliyopita, Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu mwenyewe na kukimbilia Saudi Arabia alitangaza rasmi kukabidhi madaraka kwa baraza jipya la urais lililoundwa karibuni hatua ambayo watu wengi wanasema ameichukua kwa kulazimishwa na ukoo wa Aal Saud.
Hadi alitangaza rasmi kujiuzulu Alkhamisi iliyopita ya tarehe 7 Aprili kama ambavyo alitangaza pia kumfuta kazi makamu wake, Ali Mohsen al-Ahmar.
Jumatano ya wiki iliyopita, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi lilianzisha mazungumzo mjini Riyadh kwa ajili ya Yemen, ambapo Abdrabbuh Mansur Hadi na makamu wake ambaye pia ni waziri mkuu hawakuhusishwa hatua ambayo ni udhalilishaji mkubwa kwa rais huyo wa zamani wa Yemen aliyekimbilia Riyadh kushirikiana na wavamizi wanaotenda jinai dhidi ya wananchi wa Yemen.