Serikali ya mseto ya Bennett na Lapid katika ncha ya kusambaratika
Makundi ya Waarabu ndani ya serikali ya sasa ya Tel Aviv yaani United Arab List (UAL) chama kinachowawakilisha Waarabu wanaoishi ndani ya maeneo yaliyotwaliwa na Israel chini ya uenyekiti wa Mansour Abbas mbunge wa Kiarabu ambaye pia ni mwakilishi wa muungano wa serikali ya mseto ya Israel, yametoa masharti kwa ajili ya kubakia katika baraza la mawaziri la Naftali Bennett.
Serikali hiyo ya mseto ya Naftali Bennet na Yair Lapid haijatimiza hata umri wa mwaka mmoja. Serikali hiyo inayolegalega iliundwa mwezi Juni mwaka jana na vyama vinane tofauti vya mirengo ya kati, kushoto, kulia, Waarabu na Wayahudi baada ya chaguzi nne mtawalia; na kupelekea kujiuzulu Benjamin Netanyahu baada ya miaka 12 ya kukialia kiti cha Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel.
Netanyahu alichukua hatamu za kuwa kiongozi wa upinzani dhidi ya serikali hiyo ya mseto baada ya kuondoka madarakani akiwa na ajenda ya ya kuiondoa madarakani serikali hiyo baada ya kubaini udhaifu na kulegalega kwake. Kujiuzulu Idit Silman kutoka kwenye serikali hiyo ya mseto tarehe 6 Aprili mwaka huu kuliibua mwanga wa matumaini kwa wapinzani kwa ajili ya kuipindua serikali ya sasa ya Tel Aviv. Serikali ya Bennet na Lapid iliundwa kwa kupata kura moja zaidi yaani kwa kura 61 mkabala wa kura 60 za upinzani; hivyo kujizulu ghafla kwa Silman kumelifanya Baraza la Mawaziri la Israel lipoteze wingi wa viti vya wabunge wa Knesset na hivyo viti vya uwakilishi bungeni vimegawanywa kwa usawa yaani viti 60 kwa 60 kati ya muungano tawala na kambi ya upinzani.
Benjamin Netanyahu amekaribisha hatua ya kujizulu kwa Idit Silman. Netanyahu na wafuasi wake waliandamana dhidi ya serikali ya Bennett na kutabiri kuwa serikali hiyo itaanguka hivi karibuni. Wiki mbili baada ya kujiuzulu Idit Silman muungano wa makundi ya Waarabu ambao ni kati ya wanachama wa serikali ya mseto, ulizungumzia suala la kujitoa katika serikali ya Bennett.
Imeeleza kuwa, kundi hilo limeainisha masharti kadhaa eti kwa ajili ya kubaki ndani ya muungano tawala ikiwa ni pamoja na kudumishwa hali ya sasa khususan katika Msikiti wa Al Aqsa, kuwazuia Wayahudi kuingia kufanya ibada katika viwanja vya msikiti huo, kuharakishwa suala la kuvitambua rasmi vijiji vyenye idadi kubwa ya Waarabu na kuvishughulikia huko katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Naqab pamoja na kuendeleza mradi wa kupambana na uhalifu na ghasia katika miongoni mwa jamii ya Waarabu. Kuna nukta mbili muhimu za kuzingatiwa kuhusu sababu tofauti na zenye kukikanza zilizomfanya Idit Silman kujitenga na serikali na masharti yaliyotolewa na makundi ya Waarabu kwa ajili kuendelea kuwepo katika serikali ya Naftali Bennet.
Katika uchambuzi wake, Taasisi ya Stratfor ya nchini Marekani imeandika kuwa: Sehemu ya madai iliyomfanya Idit Silman ajiuzulu ni kwamba, alihisi kuwa serikali ya Bennet haijatilia mkazo vya kutosha suala la utambulishi wa Kiyahudi ikilinganishwa na chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu. Ni wazi kuwa, Idit na wengine wenye mtazamo kama wake ndani ya serikali ya Bennett, wanataka kuzingatiwa pakubwa suala la utambulisho wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Hii ni katika hali ambayo, Orodha ya Pamoja ya Waarabu kwa upande wake inataka kupunguzwa utumiaji mabavu na jinai dhidi ya Waarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na pia kupunguzwa uzingatiaji wa kipengele cha Uyahudi ndani ya serikali. Sababu mbili hizi zinazopingana zinaonyesha kuwepo ukinzani, kukosekana umoja na kulegalega serikali ya mseto ya Bennett na Lapid.
Orodha ya Pamoja ya Waarabu (UAL) imeanishia masharti yake hayo kutokana na kiwango cha utumiaji mabavu na ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Bennett katika miezi ya karibu dhidi ya Wapalestina na Waarabu wanaoishi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Kundi hilo ambalo ina viti vinne vya uwakilishi katika Knesset, imetishia kujiuzulu kwa pamoja kutokana na kuongezeka ukandamizaji na hatua za mabavu zinaozafanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina na wakazi wengine wa Kiarabu.
Iwapo wawakilishi wa kundi hilo watajitoa katika serikali ya mseto ya Israel, idadi ya wabunge wanaoiunga mkono serikali ya Naftali Bennett itapungua na kufikia 56 kati ya viti 120 vya bunge; na hivyo kutumbukia katika hali ngumu sana. Serikali ya Bennett pia haitaweza tena kupasisha sheria yoyote na kwa msingi huo itasambaratika mapema na kabla ya muda wake kumalizika.