Barghouti: Israel imeshindwa na wanamapambano wa Palestina
Mwanasiasa wa ngazi za juu wa Palestina anasema miradi ya utawala haramu wa Israel imeporomoka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwani utawala huo ghasibu umeshindwa kukabiliana na muqawama wa Palestina.
Mustafa Barghouti, Katibu Mkuu wa chama cha kisiasa cha Ubunifu wa Kitaifa wa Palestina, ametoa kauli hiyo katika mahojiano marefu na Kanali ya Televisheni ya Al Alam ya Iran.
Baraghouthi amesema utawala wa Israel umefeli kisiasa kwani mradi wake wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya tawala za Kiarabu katika fremu ya 'muamala wa karne' haukufikia malengo yake.
Amesema uanzishaji uhusiano wa kawaida baina ya Israel na baadhi ya tawala za Kiarabu haujaweza kusababisha utengwaji wa kadhia ya Palestina kama ilivyokusudiwa.
Baraghouthi amebainisha kuwa mradi wa pili wa Israel uliofeli ni kuhusu kujumuisha masuala ya kiuchumi na amani kwani watu wa Palestina hawako tayari kukubali ardhi yao iendelee kukaliwa kwa mabavu hata kama hali yao ya kiuchumi imeboreka . Aidha amesema pamoja na kuwepo mradi huo hali ya kiuchumi ya Palestina imezorota.
Mwanasiasa huyo pia amelaani vikali ukatili wa hivi karibuni wa Palestina dhid ya Wapalestina akisema, “Mnachokiona leo ni chokochoko, mauaji, ukandamizaji na unyanyasaji ambao umefikia hatua ya dhulma na ukatili wa jinai, kama tulivyoona katika tukio la mauaji ya Ghada Sabatien, mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 46 na watoto sita. Si tu kuwa walimpiga risasi lakini pia walimwacha akivuja damu hadi kufa. Uhalifu huu hauna kifani.”
Mapema mwezi huu, Sabatien alipigwa risasi na wanajeshi wa Israel karibu na mji wa Beit Laham na kupoteza maisha baada ya kupasuka mshipa na kuvuja damu nyingi.
Alipoulizwa kama mapambano ya Palestina yamekuwa chanzo cha mkanganyiko katika vikosi vya utawala ghasibu wa Israel Barghouti alisema, "Israel inaendeleza mifumo kandamizi ili kukabiliana na upinzani wa Palestina, na Wapalestina wanaunda aina mpya za mapambano ambazo Israel haijui jinsi ya kuzidhibiti."
Kwingineko katika mahojiano hayo, Barghouti amesema kile kinachoitwa suluhisho la serikali mbili kwa suala la Palestina limeshindwa na halikubaliwi tena na Wapalestina.
Barghouti amesema gharama za kuikalia kwa mabavu Palestina na ubaguzi wa rangi ni kubwa mno kwa Israel, na kuongeza kuwa muqawama umeweka usawa wa madaraka kwa ajili ya Wapalestina.
Barghouti pia ameikosoa jamii ya kimataifa kwa kutochukua hatua katika kukabiliana na jinai za Israel, akihoji ni vipi Russia inawekewa vikwazo chungu nzima katika kipindi cha wiki chache tu huku Israel ikiwa haijaadhibiwa kwa zaidi ya miaka 74.