Kuwa tayari Lebanon kwa ajili ya zoezi la uchaguzi wa Bunge
Bassam Mawlawi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon ametangaza kuwa, maandalizi ya lazima kwa ajili ya kuendesha zoezi la uchaguzi wa Bunge nchini humo katika muda uliopangwa yamekamilika.
Duru ya 24 ya uchaguzi wa Bunge nchini Lebanon inatarajiwa kufanyika katika siku na tarehe tatu tofauti. Wananchi wa Lebanon wanaoishi katika mataifa ya Kiarabu Ijumaa ya kesho Mei 6 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi la uchaguzi wa Bunge. Tarehe 8 Mei ni siku maalumu ya Walebanon wanaoishi katika mataifa ya Magharibi kupiga kura kuwachagua wawakilishi wao wa Bunge.
Hii ni katika hali ambayo, wapiga kura ndani ya Lebanon wao wanatarajiwa kuelekea katika vituo vya kupigia kura tarehe 15 ya mwezi huu kwa minajili ya kuwachagua wawakilishi wao katika Bunge la nchi hiyo ya Kiarabu ambayo katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na jinamizi kubwa la mzozo wa kisiasa usiomalizika.
Bunge la Lebanon lina jumla ya viti 128. Kwa mujibu wa katiba ya Lebanon, nusu ya viti hivyo ni makhsusi kwa Wakristo na nusu iliyobakia ya viti hivyo ni kwa ajili ya Waislamu. Viti 64 ambavyo ni makhsusi kwa Wakristo navyo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo vina mgawanyo wake. Viti 34 wametengewa Wakristo wa Kimaroni, viti 14 kwa ajili ya Wakrsto wa madhehebu ya Orthordox, viti 8 ni maalumu kwa Wakristo wa Kikatoliki na viti vitano vimetengwa kwa ajili ya Wakristo wa Kiarmenia wa Kiorthodox, kiti kimoja kwa ajili ya Wakristo wa Kiarmenia ambao ni Wakatoliki, kiti kimoja cha Bunge kwa ajili ya Wainjilisti na kiti kimoja kilichobakia kikitengewa jamii ya Wakristo walio wachache.
Kwa upande wa Waislamu pia katiba ya Lebanon imegawanya viti 64 ambavyo ni nusu ya viti vyote vya Bunge baina ya madhehebu mbalimbali. Waislamu wa madhehebu ya Shia wametengewa viti 27 na Masuni nao wakipatiwa idadi hiyo hiyo. Jamii ya Waduruzi wamepatiwa viti 8 huku Waalawi wakitengewa viti viwili.
Jumla ya wagombea 718 wanatarajiwa kuchuana kwa ajili ya kuwania viti 128 vya Bunge la Lebanon. Bassam Mawlawi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon amesema kuwa, idadi ya wagombea imeongeza mara hii ikilinganishwa na uchaguzi wa Bunge uliopita.
Uchaguzi wa mara hii una mambo mawili muhimu.
Jambo la kwanza ni kujiondoa Saad al-Hariri ambaye ametangaza kutoshiriki katika uchaguzi huu. Saad al-Hariri, kiongozi wa mrengo wa al-Mustaqbal na Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon alitangaza huko nyuma kwamba, anasimamisha kwa muda harakati zake za kisiasa na kwamba, hatoshiriki katika uchaguzi wa Bunge wa mara hii. Baada ya msimamo huo wa al-Hariri, wanasiasa watatu mashuhuri na watajika wa Kisuni yaani Tammam Salam, Najib Mikati na Fuad Siniora nao wakatangaza kwamba, hawatagombea uchaguzi wa mara lakini wakaacha mlango wazi wa kuungwa mkono mirengo yao.

Kwa muktadha huo, kujitoa Saad al-Hariri kumeufanya ushindani katika kambi ya Masuni kuwa tata zaidi na ni vigumu mno kutabiri kwamba, viti 27 ambavyo ni kwa ajili ya Waislamu wa Kisuni vitanyakuliwa na wagombea kutoka kundi na mrengo gani.
Jambo la pili ni kuwa, uchaguzi wa Bunge nchini Lebanon unatarajiwa kufanyika katika hali ambayo wananchi wa nchi hiyo hawana matumaini kabisa ya kuboreka hali ya mambo hasa kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na mgogoro wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa pamoja na matatizo ya kisiasa yanayoisumbua nchi yao kwa miaka kadhaa sasa.
Ukweli wa mambo ni kuwa, wananchi wa Lebanon wanaamini kuwa, hali yao ya kimaisha haiwezi kubadilika na kuboreka kupitia uchaguzi. Ni kwa msingi huo, ndio maana weledi wa mambo wanatabiri kwamba, kiwango cha ushiriki katika uchaguzi huu kinatarajiwa kuwa kidogo ikilinganishwa na chaguzi za Bunge zilizotangulia.