May 20, 2022 01:20 UTC
  • Wahindu wenye misimamo mikali wateketeza moto msikiti India

Wahindu wenye misimamo mikali nchini India wameteteketeza moto msikiti kati mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Jang la Pakistan, Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada wameteketeza moto msikiti katika mji wa Nemuch katika jimbo la Madhya Pradesh. Taarifa zinasema Wahindu wenye misimamo mikali pia wamevurumisha mawe katika nyumba za Waislamu katika jimbo hilo na kuwajeruhi Waislamu kadhaa. 

Katika upande mwingine, katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa India, mwanamke Muislamu aliyekuwa na umri wa miaka 53 alipigwa risasi na kuuawa na polisi wakati akijaribu kuzuia mwanae wa kiume kukamatwa kwa kosa la kuchinja ng'ombe.

Hivi karibuni katika eneo la Karauli jimboni Rajasthan nyumba 40 za Waislamu ziliteketezwa moto na Wahindu wenye misimamo mikali.

Miaka mitatu iliyopita eneo lenye Waislamu wengi linalozozaniwa la Kashmir linalosimamiwa na India lilipokonywa mamlaka yake ya ndani na baada ya hapo serikali ikaanza kuweka vizingiti katika mijimuiko ya kidini ya Waislamu. Aidha India inatekeleza sheria yenye utata ya kutowapa uraia Waislamu wanaotajwa kuwa ni wahajiri nchini humo. Hatua hizo zinazochukuliwa na serikali ya India dhidi ya Waislamu zinaonekana ni idhini isiyo ya moja kwa moja kwa Wahindu wenye misimamo mikali kuwashambulia Waislamu wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi

Hatua mpya ya Wahindu wenye misimamo mikali ya kuteketeza moto msikiti katika mji wa Nemuch jimboni Madhya Pradesh inaonyesha kuwa, Wahindu wenye misimamo mikali ya utaifa wanatekeleza hujuma dhidi ya maeneo matakatifu ya Waislamu huku vikosi vya usalama vikiwa vimekaa kimya bila kuchukua hatua yoyote

Katika mwezi wa Aprili 2022 pia katika sherehe ya Kihindu ya "Ram Navami" katika jimbo la Madhya Pradesh, mamia ya nyumba za Waislamu jimboni humo ziliharibiwa na mabuldoza yaliyokuwa yakiendeshwa na Wahindu wenye misimamo mikali. Picha za familia zisizo na nyumba na watoto waliokuwa wakilia baada ya jinai hiyo zilisambazwa katika mitandao ya kijamii na kulaaniwa kieneo na kimataifa.

Kuteketeza moto msikiti, ambalo ni eneo takatifu kwa Waislamu, si jambo jipya nchini India.

Katika miongo ya hivi karibuni idadi kubwa ya misikiti huko India imeharibiwa, kuteketezwa moto au kuhujumiwa na Wahindu wenye misimamo mikali. Waislamu wengi wameuawa au kujeruhiwa katika hujuma hizo za Wahindu. Kwa kawaida jinai hizo hujiri baada ya hotuba za Wahindu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Disemba sita mwaka 1992, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwa lengo la kujenga hekalu la ram, moja ya miungu ya Kihindu. Katika hujuma hiyo Waislamu zaidi ya 2,000 waliuawa. 

Wahindu katika msikiti wa kihistoria wa Babri

Hakuna shaka kuwa sera za serikali ya India zimeandaa mazingira kwa Wahindu wenye misimamo mikali nchini humo kutekeleza hujuma dhidi ya Waislamu. Swali linaloibuka hapa ni hili kuwa, je, ni kwa nini chama tawala nchini India cha Bharatiya Janata (BJP) kinahimiza na kuimarisha misimao mikali ya kitaifa ya Wahindu?

Weledi wa mambo wanasema katika miaka ya hivi karibuni tokea Narendra Modi aingie madarakani kama Waziri Mkuu wa India amekuwa akilenga kuimarisha chama chake na moja ya njia za kupata nguvu zaidi ni kuhimiza misimamo mikali ya Kihindu na kuchochea hisia dhidi ya Waislamu. Katika kufikia lengo hilo, serikali ya sasa ya India imekuwa ikihimiza ujenzi wa mahekalu ya Wahindu na kuharibiwa maeneo matakatifu ya Waislamu.

 

Tags