Hamas: Utawala wa Kizayuni hauna mamlaka yoyote huko Quds
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel hauna mamlaka yoyote katika mji wa Quds na kwamba Hamas itaendelea kuupigania mji huo hadi utakapokombolewa.
Mji wa Quds ambao ndani yake kuna Msikiti Mtukufu wa al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu, ni sehemu muhimu ya Palestina na ni kati ya maeneo matukufu ya Kiislamu.
Hamas imetoa taarifa ikisisitiza kuwa: Mji wa Quds ambao ndani yake upo Msikiti wa al Aqsa, ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi za Palestina.
Harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imeongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel hauna uhalali wala mamlaka yoyote huko Quds na jitihada zote zinazofanywa na utawala huo haramu za kuvuruga utambulisho wake wa Kipalestina, Kiarabu na Kiislamu katika kipindi chote cha historia, zitagonga mwamba.
Taarifa hiyo ya Hamas ambayo imetolewa katika kumbukumbu ya kutimia mwaka wa 55 wa kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Quds Tukufu na utawala wa Kizayuni imesisitiza kuwa, mji wa Quds utaendelea kuwa mji mkuu wa milele wa Palestina na kitovu cha harakati za Umma wa Kiarabu na Kiislamu.
Hamas imetahadharisha pia kuhusu njama za kuuinguza utawala wa Kizayuni katika muundo wa Ulimwengu wa Kiarabu kupitia njia mbalimbali kama kuanzisha uhusiano wa kawaida, kuanzisha miungano na kikataba, na kushirikiana na utawala huuo katika nyanja mbalimbali na kusisitiza kuwa: inalaani hatua zote hizo kwa sababu utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia vibaya hatua za aina hiyo kuzidisha uvamizi na hujuma zake dhidi ya raia wa Palestna, ardhi na matukufu yao.