Muqtada Sadr ataka kuvunjwa bunge la Iraq na kuitishwa uchaguzi mpya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i86630-muqtada_sadr_ataka_kuvunjwa_bunge_la_iraq_na_kuitishwa_uchaguzi_mpya
Mkuu wa mrengo wa Sadr nchini Iraq ametaka kuvunjwa bunge la nchi hiyo na kutishwa uchaguzi mwingine wa haraka na wa kabla ya wakati wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2022 02:41 UTC
  • Muqtada Sadr ataka kuvunjwa bunge la Iraq na kuitishwa uchaguzi mpya

Mkuu wa mrengo wa Sadr nchini Iraq ametaka kuvunjwa bunge la nchi hiyo na kutishwa uchaguzi mwingine wa haraka na wa kabla ya wakati wake.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Muqtada Sadr amesema hayo katika hotuba yake kwa njia ya televisheni na kuongeza kuwa, baada ya kuvunjwa bunge na kuitishwa uchaguzi mpya kwa mujibu wa demokrasia, sura zote za zamani zitatoka ndani ya bunge la Iraq.

Wiki iliyopita na baada ya mkwamo wa miezi 10, Muhammad Shiya'a al Sudani aliteuliwa kugombea uwaziri mkuu wa Iraq na kupatikana matumaini ya kuundwa serikali mpya nchini humo. Lakini wakati Bunge la Iraq lilipokuwa katika mchakato wa kuchagua Rais na Naibu wa Kwanza wa Spika wa bunge hilo, wafuasi wa Muqtada al Sadr walifanya maandamano kupinga jambo hilo, wakalivamia bunge la kuzidi kutatanisha mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Muhammad Shiya'a al Sudani

 

Muqtada Sadar amedai kuwa hakuna ugomvi wa madaraka nchini Iraq, kilichopo ni kupigania haki na bado nafasi ya wananchi wa kushiriki katika uchaguzi ipo kwa ajili ya kuchagua viongozi wanaofaa zaidi. 

Baadhi ya mirengo ya Iraq imeunga mkono matamshi wa Muqtada Sadr na mingine imempinga, suala ambalo linazidi kutia wasiwasi mustakbali wa kisiasa wa Iraq.