Kushindwa chokochoko za Saudi Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati
Ukiritimba na chokochoko za Saudi Arabia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika eneo la Mashariki ya Kati vimeusababishia utawala wa kifalme wa familia ya Aal Saud matatizo makubwa yasiyo na kifani.
Robert Fisk, mchambuzi mashururi wa masuala ya Mashariki ya Kati kutoka Uingereza ameandika kwenye makala yake katika gazeti la 'Independent' kwamba, licha ya Saudi Arabia kutumia fedha nyingi katika kuyaunga mkono makundi yenye misimamo mikali katika nchi za Iraq, Yemen na Syria, bado haikuweza kufikia malengo yake na badala yake hatua hiyo imedhoofisa nafasi ya Riyadh katika siasa za kimataifa. Fisk ambaye amekuwa mwandishi wa gazeti hilo mashuhuri la Uingereza kwa zaidi ya miaka 20 na ambaye amekuwa mfuatiliaji wa siasa za Mashariki ya Kati kwa muda wote huo amesema kuwa, watawala wa Saudi Arabia wakiongozwa na Mfalme Salman bin Abdulaziz wamejikuta kwenye kinamasi baada ya kushindwa kwenye kadhia ya Yemen na Iraq na sasa wanataka kujitia kitanzi kutokana na mpango wao wa kutaka kutuma majeshi ya nchi kavu ndani ya ardhi ya Syria. Amesema hilo likifanyika, Riyadh itakuwa imefanya makosa makubwa na ya kistratejia katika siasa zake za Mashariki ya Kati. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati anasema dunia inashangazwa kuona kwamba Saudia inashikilia kutuma jeshi huko Syria wakati kila mtu anajaribu juu chini kutatua mgogoro wa nchi hiyo kupitia njia za kisiasa na kidiplomasia.
William Rugh, balozi wa zamani wa Marekani katika nchi za Yemen na Saudi Arabia amesema kwa upande wake kwamba utawala wa sasa wa Riyadh unatofautiana na wafalme waliopita na kwamba uongozi wa Salman bin Abdulaziz na mwanaye Mohamad bin Salman umeisababishia nchi matatizo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Mwanadiplomasia huyo wa zamani wa Marekani katika tathmini yake anasema, stratejia ya kijeshi ya Saudi Arabia katika nchi za Yemen na Iraq imefeli na kusisitiza kwamba, Riyadh ikiingia kijeshi Syria itapata pigo kubwa zaidi.
Ni wazi kwamba tamaa ya Saudia ya kupeleka jeshi nchini Syria ni kwa ajili ya kutaka kuleta mlingano wa nguvu katika medani ya vita baada ya kuona makundi inayoyaunga mkono yanashindwa vibaya na jeshi la serikali ya Rais Bashar Asad.
Yote hayo yanadhihirisha jinsi Saudi Arabia ilivyovuruga hali ya mambo katika Mashariki ya Kati katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Ripoti zinaonyesha kuwa, hatua ya Saudia ya kuvamia Yemen kwa kisingizio cha kutetea demokrasia imesababisha hali ya nchi hiyo kuwa mbaya na kushajiisha makundi ya kidaidi ambayo katika miezi ya hivi karibuni yameanza tena kuwahangaisha wananchi wa taifa hilo la Kiarabu.
Kinachozungumziwa na wachambuzi wengi ni kwamba, licha ya siasa hizo za kijuba na za kujitanua za utawala wa Aal Saud, bado mfalme Salman na wenaye mjini Riyadh hawajaweza kufikia hata lengo moja katika orodha ya malengo yao mengi haramu katika eneo la Mashariki ya Kati.