Mamluki wa Imarati wazidisha utekaji nyara Yemen
Vitendo vya utekaji nyara vinavyofanywa na wanamgambo mamluki wa Muungano wa Falme za Kiarabu huko Yemen vimeongezeka.
Saudi Arabia huku ikiungwa mkono kwa hali na mali na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa Machi 2015 iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga na nchi kavu; ambapo kufuatia uvamizi huo Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameuliwa na makumi ya maelfu wamejeruhiwa katika vita nchini humo na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi.
Wanamgambo mamluki wanaoungwa mkono na serikali ya Imarati katika mkoa wa Aden jana Jumatatu waliwatekanyara watu wawili wenyeji wa wa wilaya ya Ibb mkoani humo. Aidha mamluki hao wa Imarati Jumanne iliyopita walivamia hoteli moja na kuwatekanyara watu 11 wakazi wa mji wa Taiz ambao walikuwa wameelekea Aden kufuatilia pasi zao za kusafiria. Vitendo vya utekajinyara vinavyofanywa na mamluki wanaopata himaya kutoka Imarati vimeongezeka katika siku za karibuni katika mikoa ya kaskazini mwa Yemen.
Muungano wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa vya Yemen pia ulibainisha wasiwasi wake kuhusu kushtadi kwa wimbi la utekajinyara na ukosefu wa usalama katika mji wa Aden, kusini mwa Yemen na kutekwanyara wanazuoni wa kidini.
Ujumbe huo wa wanazuoni wa Yemen pia umesisitiza kuwa, utekajinyara raia na kuzusha hofu miongoni mwa watu wasio na hatia ni kinyume cha thamani za Kiislamu na maadili ya jamii ya Kiislamu ya Yemen.