ICC yatakiwa iizuie Israel kuwafukuza Wapalestina kwenye makazi yao
Kituo cha Haki za Binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) cha B'Tselem kimeiandikia barua Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kikiitaka iingilie kati na isimamishe mpango wa utawala wa Kizayuni wa kutaka kuwafurusha maelfu ya Wapalestina kwenye makazi yao.
Kituo hicho kimemtaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan achukue hatua za makusudi haraka iwezekanavyo, na kuizuia Israel kuwafukuza maelfu ya Wapalestina kwenye nyumba zao katika eneo Masafer Yatta, kusini mwa mji wa al-Khalil katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina la WAFA, vijiji 8, shule 4, kliniki kadhaa na mamia ya majengo ya makazi ya watu katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu, yanatazamiwa kubomolewa na Wazayuni maghasibu karibuni.
Kundi hilo la kutetea haki za binadamu limesema Israel kwa miongo kadhaa sasa imekuwa ikifanya jitihada za kuwafurusha Wapalestina kutoka kwenye makazi yao katika eneo la Masafer Yatta, lenye vitongoji 19 vya Wapalestina huko kusini mwa Ukingo wa Magharibi.
Kituo cha B'Tselem ambacho kinajishughulisha na upashaji taarifa kuhusu haki za binadamu huko Israel kimesema wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na jinamizi mbalimbali kutoka kwa Wazayuni, kuanzia kubughudhiwa na askari wa utawala huo pandikizi, kuhujumiwa haki zao za faragha, mbali na kuandamwa na matatizo ya kimazingira.
Mei mwaka huu 2022, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilikosoa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Israel, wa kutupilia mbali rufaa ya kupinga agizo la kufukuzwa Wapalestina kutoka kwenye makazi yao eneo la Masafer Yatta.