Rais wa Iran aipongeza Iraq kwa kuchagua rais mpya
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza serikali na wananchi wa Iraq, kufuatia kuchaguliwa na Bunge, Abdul Latif Rashid kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika salamu zake za pongezi, Rais wa Iran amesema anatumai kuchaguliwa Abdul Latif Rashid kuwa rais mpya wa Iraq itakuwa hatua moja mbele kuelekea kwenye Iraq iliyostawi na kushamiri.
Amesema ana matumaini kuwa uchaguzi huo utafungua zaidi milango ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Iran na Iraq katika nyuga mbalimbali.
Rais Raisi sambamba kuitakia kheri na fanaka serikali mpya ya Baghdad na wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu amesisitiza kuwa, taifa la Iran daima limekuwa likiunga mkono mieleko ya kisiasa ya Iraq iliyojengwa kwenye misingi ya irada ya wananchi.
Bunge la Iraq hapo jana lilimchagua Abdul Latif Rashid mwenye umri wa miaka 78, kuwa rais mpya wa nchi hiyo baada ya kuzoa kura 160. Wabunge 269 kati ya 329 wa Bunge la Iraq walishiriki zoezi hilo la upigaji kura jana alasiri.
Taifa hilo la Kiarabu limekuwa katika mvutano wa kisiasa, uliopelekea kushindwa kuunda serikali tangu baada ya uchaguzi wa Bunge wa Oktoba mwaka jana.
Mwanasiasa huyo Mkurdi anakuwa rais wa nne wa Iraq, na anakuja kurithi mikoba ya Barham Salih, ambaye aliambulia kura 99 katika zoezi hilo la jana.
Tayari Rais Rashid amemteua Mohammed Shia al-Sudani mwenye miaka 52 kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, kujaza nafasi ya Mustafa al-Kadhemi.