Oct 29, 2022 04:21 UTC
  • HAMAS, Jihad Islami na Yemen zalaani shambulio la kigaidi nchini Iran

Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina na mamlaka za Yemen zimetoa taarifa za kulaani shambulio la kigaidi lililotokea siku ya Jumatano katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh ya mjini Shiraz, kusini magharibi mwa Iran.

Jana Ijumaa, Harakati ya Muqawama wa Palestina ya Jihad Islami ilitoa taarifa ya kulaani shambulio hilo la kigaidi, ambalo genge la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika nalo.

Taarifa ya harakati hiyo imesema: Operesheni za kigaidi za namna hii zinafanyika kwa lengo la kuuondoa Ulimwengu wa Kiislamu kwenye njia ya mafundisho sahihi ya Uislamu.

Nayo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa taarifa ya kulaani hujuma hiyo ya kigaidi, sanjari na kulinyooshea taifa la Iran mkono wa pole kufuatia shambulio la umwagaji damu.

Wakati huohuo, Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen limekosoa vikali uhaini huo, na kulitaja shambulio hilo la kigaidi kuwa la kioga.

Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema katika taarifa kuwa: Kuwalenga wanawake, wazee na watoto ni jinai ya kihaini inayokwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.  

Wairani katika maandamano ya kulaani shambulio la kigaidi na kutangaza uungaji mkono kwa serikali

Hadi hivi sasa nchi mbalimbali duniani zimeshatoa mkono wao wa pole kufuatia shambulio hilo la kigaidi la Jumatano iliyopita, ambapo watu wasiopungua 15 waliuawa shahidi huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.

Miongoni mwa nchi hizo ni Russia, China, Uturuki, Pakistan, Armenia, Jamhuri ya Azerbaijan, Misri, Imarati, Venezuela, Oman, Syria, Iraq, Finland, Umoja wa Mataifa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Kataib Hizbullah ya Iraq, Ansarullah ya Yemen n.k, zimetoa mkono wa rambirambi kwa serikali na taifa la Iran kufuatia jinai hiyo iliyofanywa na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).

Tags