Watu 53 wasubiri kunyongwa kwa umati Saudia, Magharibi kimya! + VIDEO
(last modified Tue, 01 Nov 2022 11:17:19 GMT )
Nov 01, 2022 11:17 UTC
  • Watu 53 wasubiri kunyongwa kwa umati Saudia, Magharibi kimya! + VIDEO

Nchi za Magharibi zimeendelea kunyamazia kimya taarifa kuwa Saudi Arabia imepanga kuwanyonga kwa umati watu 53 nchini humo. Kwa uchache wanane kati ya watu hao ni watoto wadogo.

Taasisi moja ya barani Ulaya ya kufuatilia haki za binadamu nchini Saudia imefichua kuwa hivi sasa watu 15 wengine wanasubiri kunyongwa na kuifanya idadi ya Wasaudia wanaosubiri kunyongwa kwa umati kufikia 53.

Hukumu hiyo imetolewa huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni wakiitaka serikali ya Saudi Arabia imwachilie huru Abdullah al-Hawaiti haraka iwezekanavyo kutokana na kuwa alipachikwa tuhuma hizo akiwa bado mtoto mdogo.

Taasisi hiyo ya haki za binadamu imewanukuu wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakitoa taarifa hiyo kutokana na kuendelea kuhatarishwa maisha ya makumi ya watu wakiwemo watoto kadhaa na wameionya serikali ya Saudia isifanye jinai nyingine mpya.

Wasiwasi wa duru na asasi za kimataifa kuhusu uwezekano wa kutendwa jinai nyingine na ukoo wa Aal Saud unatokana na ukweli kwamba utawala huo wa kiimla una rekodi iliyojaa jinai za mauaji ya halaiki na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mwezi Machi mwaka jana, utawala wa Aal Saud katika jinai ya kutisha, utawala wa kidikteta wa Saudia uliwanyonga kwa umati watu 81 katika siku moja tu tena baadhi yao wakiwa ni raia wa nchi nyingine kama Yemen. 41 kati ya watu hao 81 walionyongwa kwa halaiki na ukoo wa Aal Saud walikuwa Waislamu wa madhehebu ya Kishia.

Jinai zote hizo zinafanyika huku nchi za Magharibi zinazojidai kulinda na kupigania haki za binadamu zikiendelea kukaa kimya kama vile hakuna chochote kinachotokea. Ni wazi kabisa kwamba lau si uungaji mkono usioyumba wa Marekani na nchi za Magharibi kwa ukoo wa Aal Saud, utawala wa kiimla wa Saudi Arabia usingethubuti kufanya mauaji hayo.