Shtayyeh: Serikali mpya ya Israel inajiandaa kutangaza vita dhidi ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i90836-shtayyeh_serikali_mpya_ya_israel_inajiandaa_kutangaza_vita_dhidi_ya_wapalestina
Waziri Mkuu wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, serikali mpya ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel chini ya uongozi wa wanasiasa wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu ada inajiandaa kutangaza vita dhidi ya Wapalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 22, 2022 08:01 UTC
  • Shtayyeh: Serikali mpya ya Israel inajiandaa kutangaza vita dhidi ya Wapalestina

Waziri Mkuu wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, serikali mpya ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel chini ya uongozi wa wanasiasa wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu ada inajiandaa kutangaza vita dhidi ya Wapalestina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina SAMA, Muhammad Ashtiyeh, amebainisha kuwa mazungumzo ya uundaji baraza la mawaziri la Israel yanafanyika kwa msingi wa kuhakikisha ni nani ataweza kujenga vitongoji zaidi vya walowezi wa Kizayuni na nani anayetaka kurahisisha kazi ya kuwafyatulia risasi Wapalestina na kutaifisha ardhi nyingi zaidi za Wapalestina.

Ashtiyeh ameongeza kuwa, tangu ulipoanza mwaka huu wa 2022, zaidi ya watoto 40 Wapalestina wameuawa shahidi, na zaidi ya kesi 750 za kukamatwa watoto wadogo zimerekodiwa, na kungali kuna takriban watoto 160 wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala huo ghasibu.
Muhammad Ashtiyeh

Tarehe 13 Novemba, rais wa utawala wa Kizayuni Yitzhak Herzog alimkabidhi rasmi Benjamin Netanyahu, kiongozi wa muungano wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mpaka jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri.

Kwa mujibu wa sheria za utawala wa Kizayuni, Netanyahu ana muda wa siku 28 za kuunda serikali yake, na endapo italazimu ataweza kurefusha muhula huo kwa siku nyingine 14.
Tangu kufichuliwa ufisadi wa Netanyahu na kufikishwa mahakamani miaka minne iliyopita, wingu la mtikisiko wa kisiasa limeugubika utawala wa Kizayuni ambapo katika kipindi hicho zimefanyika chaguzi tano za bunge la utawala huo haramu.../