Jun 14, 2016 08:04 UTC
  • Upinzani wa Israel kwa mpango wa amani wa Waarabu

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesisitiza kwa mara nyengine tena kuwa anapinga mpango wa amani uliopendekezwa na nchi za Kiarabu.

Benjamin Netanyahu, amerudia kauli yake hiyo alipohutubia kikao cha mawaziri kutoka chama chake cha Likud na kueleza kwamba nchi za Kiarabu zinapaswa kuufanyia marekebisho kadhaa mpango huo kulingana na matakwa ya Israel na kwamba endapo hilo litafanyika ndipo itawezekana kuanza mazungumzo.

Netanyahu amesisitiza kuwa kutokana na nukta hasi zilizomo kwenye mpango wa amani wa Waarabu kwa mtazamo wa utawala wa Kizayuni, ikiwemo ya kurudi kwenye mipaka ya mwaka 1967 na kutakiwa Israel iondoke katika baadhi ya maeneo ya ardhi za Palestina, haiwezekani kwa namna yoyote ile kuukubali mpango huo wa amani uliopendekezwa na nchi za Kiarabu na kuutumia kama msingi wa mazungumzo na Wapalestina.

Kwa kutaka yafanyike mabadiliko katika mpango wa amani uliopendekezwa na nchi za Kiarabu ya kufuta hata haki chache walizorejeshewa Wapalestina, utawala haramu wa Kizayuni unataka kuzikubalisha nchi za Kiarabu suala la kutambuliwa rasmi na nchi hizo utawala huo ghasibu kuwa dola la Kiyahudi, ili kwa njia hiyo kuifuta kikamilifu haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea kwenye ardhi walikozaliwa.

Hii ni katika hali ambayo suala la kubadilishana ardhi, ambalo ni miongoni mwa ajenda kuu za harakati eti za kusaka amani Mashariki ya Kati, nalo pia limo kwenye mpango wa amani wa Waarabu; na lengo lake ni kuandaa mazingira ya kuuwezesha utawala wa Kizayuni kuyapora na kuyadhibiti maeneo zaidi ya Wapalestina na kuupa uhalali wa kisheria utawala huo vamizi katika eneo.

Katika mazingira kama hayo Netanyahu amesisitiza kwamba, nukta chanya katika mpango huo kwa mtazamo wa Israel ni kuwa tayari nchi za Kiarabu kufikia makubaliano ya amani na Israel na kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo.

Mpango wa amani wa Waarabu ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza na Saudi Arabia mwaka 2002 unajumuisha ndani yake hati jumuishi ya makubaliano ya amani ya nchi 22 za Kiarabu na utawala wa Kizayuni na kutambuliwa rasmi utawala huo na nchi hizo mkabala na utawala wa Kizayuni kurejea kwenye mipaka ya kabla ya mwaka 1967.

Kunyamaziwa kimya haki ya wakimbizi Wapalestina kurejea makwao pamoja na suala la wafungwa Wapalestina ni sehemu tu ya fursa kubwa za upendeleo ambazo nchi wafanya mapatano za Kiarabu zimeupatia utawala wa Kizayuni.

Utawala wa Kizayuni ambao unapinga kutoa hata haki chache za Wapalestina, mara tu ulipotangazwa mpango wa amani wa Waarabu uliupinga, na kwa sababu hiyo mpango huo nao ukaishia kwenye mkwamo.

Katika miaka ya karibuni, Marekani na nchi kadhaa za Kiarabu zinazoshabikia kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni pamoja na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamejaribu kutumia kila mbinu za kuufanyia marekebisho mpango wa amani wa Waarabu ili kuzifuta hata hizo haki chache zilizosalia za Wapalestina.

Njama hiyo imezidisha malalamiko ya Wapalestina na fikra za waliowengi wanaopinga mchakato wa mapatano na utawala wa Kizayuni ambao hauna lengo jingine ghairi ya kupora haki zote za Wapalestina.

Hakuna shaka yoyote kuwa kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni hakuna tija nyengine zaidi ya kuufanya utawala huo ujipanue zaidi na kuwafanya viongozi wake wawe na jeuri na kiburi zaidi cha kuhakikisha wanapora haki zote za wananchi madhulumu wa Palestina. Matamshi aliyotoa Netanyahu yanapasa kutathminiwa katika muelekeo huo.../

Tags