Indhari ya UN: Njaa inatishia maisha ya mamilioni ya Wasyria
(last modified Sun, 29 Jan 2023 07:48:33 GMT )
Jan 29, 2023 07:48 UTC
  • Indhari ya UN: Njaa inatishia maisha ya mamilioni ya Wasyria

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetahadharisha kuhusu hatari inayotishia maisha ya mamilioni ya wananchi wa Syria kutokana na ukosefu wa chakula na njaa.

Tokea mwaka 2011 hadi sasa Syria imeathiriwa na mgogoro wa mchafuko na ukosefu wa amani uliosababishwa na hujuma ya makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na kusaidiwa kwa hali na mali wa Marekani, nchi za Ulaya na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, na pia utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Shirika la WFP limetangaza katika taarifa yake kuwa Syria imekumbwa na njaa kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Syria imeathirika pakubwa kiuchumi baada ya miaka 12 ya mapigano nchini humo huku raia milioni 12 wakiwa hawajui wapi watapata mlo wao wa chakula kwa siku.  

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeongeza kubainisha kuwa, Wasyria miioni 2.9 wanakabiliwa na hatari ya njaa na hii ina maana kuwa asilimai 70 ya wananchi wa Syria siku chache zijazo huwenda wakashindwa kujidhaminia chakula cha familia.   

Syria inashika nafasi ya sita duniani kwa uhaba wa chakula. David Beasley Mkurugenzi Mtendaji wa WFP amesema akiwa ziarani mjini Damascus, kwamba, hali ya mambo itakuwa mbaya sana huko Syria iwapo hakutapatikana njia ya kutatua mgogoro wa kibinadamu unaotatiza nchi hiyo." 

David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP

Beasley ametahadharisha pia kuwa kuna uwezekano wa kushuhudiwa wimbi jipya la wakimbizi sawa na  hali ile iliyoikumba Ulaya mwaka 2015. "Je  hiki ndicho ambacho jamii ya kimataifa inakitaka?" amehoji Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP).