Amnesty International: Saudia inaitumia vibaya michezo kufunika jinai zake
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa utawala wa Saudi Arabia unaitumia vibaya michezo kuficha rekodi yake chafu, ya maafa na ya kutisha ya haki za binadamu.
Kila mwaka utawala wa Saudia hutoa hukumu za adhabu za vifungo vya muda mrefu jela na za kifo kwa wapinzani wa utawala huo kwa lengo la kukabiliana na uhuru wa kujieleza na kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Kufuatia kuanza kwa malalamiko na maandamano makubwa hususan katika maeneo ya Waislamu wa madhehebu ya Shia mashariki mwa Saudi Arabia mwaka 2011 ya kupigania usawa, uadilifu wa kijamii na kukomeshwa ubaguzi na unyanyasaji wa kimadhehebu,imekuwa ni kawaida kwa mamlaka na vyombo vya usalama vya Saudia kuwalenga kwa mpangilio maalumu watu wa maeneo hayo kwa kuwashambulia, kuwaweka kizuizini na hata kuwanyonga.
Felix Jakens, mkuu wa operesheni za kipaumbele za Amnesty International na watu walio hatarini, ameliomba Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) litangaze hadharani kuhusu ulazima wa kufanywa mageuzi katika uwanja wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia na kutoruhusu utawala wa Riyadh uyatumie vibaya kwa maslahi yake mashindano ya Kombe la Dunia la kwanza la Wanawake, yaliyopangwa kufanyika nchini Australia na New Zealand kuanzia Julai 20 hadi Agosti 20, 2023 kuficha sura yake ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Felix Jekins ameongeza kuwa, baada ya kusaini mkataba na mwanasoka wa Ureno Cristiano Ronaldo, kuinunua klabu ya soka ya Newcastle United na LIV Golf pamoja na kuandaa matukio mengi ya michezo katika ngazi ya juu, Saudia inataka kuitumia michezo kwa manufaa yake ili kuficha rekodi yake mbaya na chafu ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Kuhusiana na hili, mashirikisho ya soka ya Australia na New Zealand yametoa taarifa ya pamoja na kutangaza kwamba yamefadhaishwa na kushutushwa na hatua ya Saudi Arabia ya kudhamini mashindano ya Kombe la Dunia ya Wanawake 2023.../