HAMAS: Njama za Marekani za kuisambaratisha Intifadha zitafeli
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS amesema njama za Marekani za kutaka kuisambaratisha Intifadha ya Tatu ya Wapalestina dhidi utawala wa Kizayuni wa Israel zitagonga mwamba.
Abdel Latif al-Qanou amesema hayo katika taarifa na kusisitiza kuwa, Washington kamwe haiwezi kuwaburuza Wapalestina na kuwalazimisha waachane na mapambano yao ya halali dhidi ya Wazayuni katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu.
Ameeleza bayana kuwa, "Intifadha na mapambano ya Wapalestina dhidi ya Wazayuni yataendelea bila kikomo katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa, na Wapalestina wataendelea kupigania ardhi na matukufu yao."
Msemaji wa HAMAS amesisitiza kuwa, Wazayuni na Wamarekani wanatiwa kiwewe na Intifadha na mwamko mpya wa Wapalestina katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Amesema muqawama ndiyo njia na chaguo pekee la taifa la Palestina katika kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba, wananchi wa Palestina wataendeleza kwa nguvu zote jitihada na mapambano ya kulikomboa kikamilifu taifa lao kutoka kwenye makucha ya utawala haramu wa Israel.
Viongozi kadhaa wa kisiasa wa Palestina wamekuwa wakisisitiza kuwa, Intifadha ya Wapalestina itaendelea hadi ukombozi utakapopatikana, nahadi pale utakapofutwa uamuzi uliotangazwa na aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump wa kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.