Gazeti la Oman: Wakati umewadia wa nchi za Kiarabu kurejea Syria
(last modified Tue, 21 Feb 2023 10:55:49 GMT )
Feb 21, 2023 10:55 UTC
  • Gazeti la Oman: Wakati umewadia wa nchi za Kiarabu kurejea Syria

Kufuatia safari ya Rais Bashar al Assad wa Syria nchini Oman na mazungumzo aliyofanya mjini Muscat na Sultan Haitham bin Tariq wa nchi hiyo gazeti moja la nchi hiyo limeandika kuwa wakati umewadia kwa nchi za Kiarabu kurudi Syria na kuanzisha tena uhusiano wa kawaida na nchi hiyo ya Kiarabu.

Rais Bashar al Assad wa Syria, jana Jumatatu alielekea mjini Muscat ambako alikutana na kufanya mazungumzo na mfalme wa nchi hiyo Sultan Haitham bin Tariq.
Katika tahariri yake ya leo, gazeti hilo la Kiarabu linalochapishwa nchini Oman limehoji, "Je, Waarabu hawawajibiki kwa sehemu ya kile kilichotokea na kinachotokea nchini Syria?" na likaendelea kuandika: "tangu ulipoanza mgogoro wa Syria mwaka 2011, badala ya nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kusimama pamoja kuiunga mkono Syria na kutetea umoja wa ardhi yake, wengi wao walipiga kura ya kusimamisha uanachama wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu".
Tahariri ya gazeti hilo la Oman imeashiria kuwa Israel ndiyo pekee inayonufaika na mgogoro wa Syria na kusisitiza kwamba, katika wakati huu, vyombo vya habari na mashirika ya habari hayatoi tamko lolote hata kwa sura ya taratibu za kidiplomasia la kulaani mashambulizi ya Israel yanayokiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi ya Kiarabu.
Sultan Haitham bin Tariq wa Oman (kulia) katika mazungumzo na Rais Bashar al Assad wa Syria mjini Muscat

Wakati Rais Bashar al Assad wa Syria na ujumbe alioandamana nao walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat jana Jumatatu, walilakiwa na mfalme wa Oman Sultan Haitham bin Tariq.

Baadaye viongozi hao wawili walifanya mazungumzo ya ana kwa ana katika kasri la kifalme la Beit al-Baraka huko Seeb, karibu na Muscat, ambapo mfalme wa Oman alitoa rambirambi zake kwa serikali na taifa la Syria kufuatia janga la tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo.

Mfalme wa Oman vile vile alisisitiza uungaji mkono usioyumba wa nchi yake kwa Syria kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi na athari za hujuma za makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na madola ya kigeni pamoja na vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Damascus.

Kwa upande wake, Assad alitoa shukrani zake kwa mfalme wa Oman, mamlaka na watu wa nchi hiyo kwa mshikamano wao na Syria pamoja na misafara ya misaada ya kibinadamu iliyotumwa kuisaidia nchi hiyo. Pia alishukuru uungaji mkono wa Oman kwa Syria katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi ya ukufurishaji.

Oman ilikuwa moja ya mataifa machache ya Kiarabu yaliyodumisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Syria baada ya kuanza hujuma za makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu mwezi Machi 2011 licha ya mashinikizo ya Marekani na washirika wengine wa makundi hayo ya kigaidi katika Ghuba ya Uajemi.../

Tags