Sababu za Saudia kufikia makubaliano na Iran
Iran na Saudi Arabia zimekubaliana kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka 7 na kuamua kufungua tena balozi zao katika muda wa miezi miwili ijayo.
Uhusiano wa Iran na Saudi Arabia ulikatwa na Riyadh mwaka 2016, na katika miaka iliyofuata, serikali ya Saudia ikachukua hatua nyingi za uadui na uhasama dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kujiunga na Marekani na Israel katika kile lilichotajwa kuwa mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa tovuti ya Hill, ingawa Iran na Saudi Arabia hazijawahi kukabiliana moja kwa moja katika medani ya vita, lakini zimekuwa zikikabiliana kupitia migogoro na vita vya niaba. Sasa swali muhimu linaloulizwa hapa ni kuwa je, ni kitu gani kimeifanya Saudi Arabia kugeuka ghafla na kuamua kurejesha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kupita miaka saba?
Jibu la kwanza ni kwamba matukio na mambo katika Mashariki ya Kati hayajakwenda kama walivyokuwa wamepanga watawala wa Saudia. Mtazamo na dhana ya watawala hao hususan Mohammad bin Salman ni kwamba walidhani kuwa kwa kufuata siasa za hujuma na kushirikiana kwa karibu na Israel na Marekani, wangeweza kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iachane na siasa zake za busara katika eneo. Kilichotokea kivitendo ni kinyume kabisa na walivyotarajia watawala hao ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wake wamepata nguvu zaidi kuliko hapo awali, mfano wa hilo ukionekana wazi katika vita vya Yemen.
Jibu nyingine ni kwamba Saudi Arabia imefikia uamuzi kwamba sera zake hizo za hujuma na uhasama sio tu hazihudumii maslahi yake, bali zinawafanya washindani wake wa Kiarabu katika eneo kuipiga kumbo na kuwapa nafasi bora zaidi katika masuala ya kieneo. Wakati huo huo, Saudi Arabia inahitaji utulivu na usalama wa ndani na pia katika uhusiano wake na nchi nyingine ili kutimiza mpango wake wa 2030.
Sababu ya tatu ni kwamba Riyadh imetambua kwa kuchelewa kwamba siasa zake za kigeni za kucheza katika uwanja wa Marekani sio tu hazilindi maslahi yake, bali pia zinadhalilisha utambulisho wake na kwamba Marekani inaitumia kimaslahi tu nchi hiyo ya Kiarabu.
Sababu ya nne muhimu ni kwamba Saudi Arabia imetambua ukweli wa mambo kuhusu hali ya utawala wa Kizayuni. Leo, utawala huo ghasibu unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani kwa namna ambayo hata viongozi wake wanaonya juu ya hatari ya kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe na hatimaye kuutukomeza kabisa. Aidha, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hata lobi za Wayahudi hazikuweza au hazikutaka kuchukua hatua ya kupunguza mvutano uliokuwepo kati ya Washington na Riyadh.
Sababu ya tano ni uwezo na nafasi ya kieneo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Bila shaka Iran, Saudi Arabia na Uturuki ni madola matatu makuu ya Kiislamu, ambayo kila moja ina uwezo mkubwa wa kupenya katika eneo na kuzima njama yoyote ile. Kwa hivyo, kufanya uadui na Iran sio tu kwamba hakudhamini maslahi ya Saudi Arabia, bali pia kunaisababishia hasara na matatizo makubwa nchi hiyo inayoongozwa kifalme.
Mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Kipalestina Wissam Abu Shamaleh anaandika kwamba inaonekana kuwa Saudi Arabia imetambua makosa yake ya kuchukua misimamo ya uadui na uhasama katika eneo kama vile kuanzisha vita haribifu na visivyo na maana dhidi ya Yemen na sasa inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kujinasua kutoka kwenye kinamasi hicho. Pia, Wasaudia wanaona kwamba wanahitaji kubadili mtazamo wao wa huko nyuma ili kupanua uhusiano wao wa kisiasa na kiuchumi na nchi za kieneo na kimataifa. Wamefikia natija kwamba wanapaswa kuimarisha uhusiano wao na nchi za Mashariki na hasa muungano wa Russia, China na Iran, na wakati huo huo kulinda ushirikiano wao wa kistratijia na nchi za Magharibi hususan Marekani.