Kuuliwa shahidi Wapalestina 88 katika muda wa chini ya miezi 3
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa wanajeshi wa utawala haramu wa Kizayuni wamewaua shahidi Wapalestina 88 tangu kuanza mwaka huu wa 2023 hadi sasa.
Jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina zimekuwa zikiongezeka siku baada ya siku tangu mwezi Septemba mwaka 2020 kufuatia kutiwa saini mapatano ya kuhuisha uhusiano kati ya utawala wa Kizayuni na nchi kadhaa za Kiarabu. Aidha jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina zimeongezeka zaidi tangu ilipooingia madarakani serikali mpya ya Benjamin Netanyahu mwishoni mwa Septemba mwaka jana. Sababu kuu ya kuongezeka jinai hizo ni kuwa, serikali mpya ya utawala wa Kizayuni ni yenye kufurutu ada pakubwa huku mtu kama Itmar Ben Guer Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel akidhihirisha waziwazi chuki na mielekeo mikali dhidi ya Waarabu na hasa Wapalestina. Ndio maana katika muda wa chini ya miezi 3 ya karibuni serikali ya Netanyahu imepasisha mipango kadhaa dhidi ya Wapalestina; ambapo hatua hiyo imechochea kuongezeka ukandamizaji na hatua za mabavu za Wazayuni dhidi ya Wapalestina na kuuliwa shahidi na kujeruhiwa mamia ya raia hao.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, wanajeshi wa Israel wamewaua Wapalestina 88 tangu kuanza mwaka huu wa 2023; ambapo watoto 17 na mwanamke 1 ni miongoni mwa mashahidi hao. Kwa ibara nyingine ni kuwa, watoto wa Kipalestina ni moja ya tano ya mashahidi hao waliouawa na utawala wa Kizayuni katika kipindi cha chini ya miezi 3 ya karibuni katika maeneo mbalimbali huko Palestina. Pamoja na hayo yote, lakini si taasisi za kimataifa wala madola yanayodai kutetea haki za binadamu duniani yaliyochukua hatua dhidi ya jinai za Wazayuni mkabala wa watoto wa Kipalestina. Kukaa kimya kwa wale wote wanaodai kutetea haki za binadamu mkabala wa mauaji ya watoto wa Kipalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kunadhihirisha kuwa kuunga mkono suala la haki za binadamu na hasa haki za watoto si jambo mahsusi kwa watoto wote duniani bali linawahusu wale wanaopata himaya na kuungwa mkono na nchi za Magharibi. Suala hili kwa mara nyingine tena linathibitisha wazi mtazamo wa upendeleo wa Wamagharibi kuhusu haki za binadamu duniani.
Suala jingine ni kuwa, Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza idadi ya mashahidi ofauti kama ifuatavyo: Mashahidi 35 waliuliwa katika mji wa Jenin, 21 katika mji wa Nablus, mashahidi 7 huko Hebron, mashahidi waliuliwa katika mji wa Quds, 5 huko Jeriko na Aghwar, mashahidi 5 katika eneo la Qalqilyah, mashahidi 3 katika mji wa Ramallah na al Bizah, mashahidi 2 katika Ukanda wa Ghaza, 2 huko Bait-laham, shahidi mmoja huko Salfit na mwingine huko Tubas kaskazini mashariki mwa Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa katika muda wa karibu miezi 3 ya karibuni ni raia wawili tu wa Palestina waliouawa shahidi katika Ukanda wa Ghaza na waliobaki waliuliwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwa ibara nyingine ni kuwa, kuwepo idadi kubwa ya mashahidi wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi ni ishara kwamba Ukingo wa Magharibi rasmi sasa unashuhudia mapambano ya silaha. Kushuhudiwa mapambano ya silaha huko Ukingo wa Magharibi pia kunamaanisha kuwa mosi, vita dhidi ya Israel haviishii tu kwa makundi ya muqawama katika Ukanda wa Ghaza; na pili ni kwamba, Wapalestina wamefikia natija hii kuwa, kufikia mapatano na Israel hakudhamini maslahi yao bali wamechagua njia ya mapambano dhidi ya utawala huo ghasibu. Wakati huo huo, kujiri mapambano ya silaha katika eneo la Ukingo wa Magharibi kunamaanisha kudhoofika nafasi ya Mamlaka ya Ndani miongoni mwa Wapalestina. Hii ni kwa sababu, serikali hiyo ya ndani ya Palestina kimsingi haiyaamini mapambano bali inasisitiza kufikia mapatano ya udhalilishaji na utawala wa Kizayuni.