Watoto; wahanga wakuu wa vita vya miaka 8 nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95566-watoto_wahanga_wakuu_wa_vita_vya_miaka_8_nchini_yemen
Mwaka wa 8 wa vita dhidi ya Yemen umemalizika huku takwimu zikionyesha kuwa, kwa wastani, mtoto mmoja wa Yemen anafariki dunia kila baada ya dakika 10 katika vita hivyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2023 03:50 UTC
  • Watoto; wahanga wakuu wa vita vya miaka 8 nchini Yemen

Mwaka wa 8 wa vita dhidi ya Yemen umemalizika huku takwimu zikionyesha kuwa, kwa wastani, mtoto mmoja wa Yemen anafariki dunia kila baada ya dakika 10 katika vita hivyo.

Vita dhidi ya watu wa Yemen vilianza Machi 26, 2015, na sasa vimekamilisha mwaka wa nane. Vita hivyo vimetajwa na Umoja wa Mataifa kuwa maafa makubwa zaidi ya binadamu katika karne ya 21. Hapana shaka kuwa, watoto ni miongoni mwa wahanga wakuu wa vita vya Yemen.

Shirika la haki za binadamu la "Intisaf" linalofanya kazi katika uwanja wa haki za wanawake na watoto, lilitangaza katika ripoti mwishoni mwa Februari 2023 kwamba katika siku 2900 za vita huko Yemen, wanawake na watoto elfu 13, 482 wameuawa au kujeruhiwa kama matokeo ya uvamizi wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo. Ripoti hiyo ilisema, zaidi ya wanawake milioni nane wanahitaji huduma za kuokoa maisha yao, na watoto milioni 12.6 wanahitaji aina fulani ya misaada ya kibinadamu.

Mwishoni mwa mwaka wa nane wa vita vya Saudia na washirika wake nchini Yemen, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya watoto milioni 11 nchini humo na kuonya kuwa, kwa wastani, mtoto mmoja wa Yemen hufariki dunia kila baada ya dakika 10 kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.

Watoto ndio wahanga wakuu wa vita vya Yemen

Kuuawa sio hatima pekee ya watoto wanaoendelea kukabiliwa na masaibu wa Yemeni katika vita vinavyoendelea nchini humo. Magonjwa hatari, utapiamlo na ukimbizi ni miongoni mwa majanga ambayo watoto wa Yemen wanakumbana nayo kutokana na vita vya miaka 8. Kuhusiana na hilo, UNICEF ilitangaza katika taarifa yake kwamba hivi sasa "zaidi ya watoto 540,000 walio chini ya umri wa miaka mitano" nchini Yemen wanasumbuliwa na "utapiamlo mkali na wa kutisha".

Ni wazi kwamba, athari mbaya za vita na mzingiro zitaendelea kuwaandama watoto wa Yemen hata baada ya kumalizika vita hivyo. Baadhi ya watoto wa Yemen wamepoteza familia zao kabisa na wengine wamepoteza baadhi ya wanafamilia. Baadhi yao wamepata ulemavu wa viungo kutokana na kushambuliwa moja kwa moja, huku wengine wakiacha masomo na kwenda kufanya kazi ili kujikimu kimaisha baada ya wazazi wao kukatiwa mishahara. Watoto wengine wa Yemen wamepatwa na maradhi ya aina mbalimbali kutokana na ukosefu wa chakula na dawa kunakosababishwa na mzingiro wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo. Mbali na madhara ya kimwili, vita vya Yemen pia vitakuwa na athari haribifu kwa nafsi na roho za watoto ambazo yumkini zikaandamana nao kwa muda mrefu.

Kuhusiana na suala hilo, Ahmad Abu Hamra, mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Ain amesisitiza kuwa, idadi ya watoto waliouawa shahidi wa Yemen kutokana na mashambulizi ya moja kwa moja ya anga na mizinga ya muungano wa vita wa Saudia imefikia mashahidi 4,061 na idadi ya waliojeruhiwa ni 4,739. Ameongeza kuwa: Kwa kutilia maanani idadi kubwa ya watoto waliouawa shahidi na waliojeruhiwa katika kipindi cha miaka minane ya uvamizi wa Saudia na athari mbaya za muda mrefu za vita hivyo, haiwezekani kudhani kwamba walilengwa na kushambuliwa kimakosa.

Maelfu ya watoto wa Yemen wameuwa katika mashambulizi ya Saudia na washirika wake

Jambo la mwisho ni kwamba, licha ya madhara makubwa yaliyosababishwa na vita hivyo kwa watoto wa Yemen, mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa hayakuchukua hatua yoyote kuwasaidia watoto wanaoendelea kudhulumiwa wa Yemen.