Taliban: Waafghani ndio walengwa wakuu wa mashambulio ya DAESH (ISIS)
(last modified Tue, 28 Mar 2023 11:42:58 GMT )
Mar 28, 2023 11:42 UTC
  • Taliban: Waafghani ndio walengwa wakuu wa mashambulio ya DAESH (ISIS)

Naibu Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Taliban anayehusika na masuala ya kisiasa amesema, wananchi wa Afghanistan ndio walengwa wakuu wa hujuma na mashambulio ya kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).

Jana Jumatatu, watu sita waliuawa na wengine 14, akiwemo mtoto, walijeruhiwa katika shambulio la kujitoa mhanga karibu na Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya mpito ya Taliban nchini Afghanistan.
Kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) limetangaza leo kupitia mtandao wa kijamii kuwa mmoja wa washambuliaji wa kujitoa mhanga wa kundi hilo ndiye aliyehusika na mripuko huo karibu na Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya muda ya Taliban mjini Kabul.
Maulavi Abdul Kabir, Naibu waziri mkuu serikali ya muda ya Taliban anayehusika na masuala ya kisiasa amesema kuhusiana na shambulio hilo la jana kwamba "kazi ya kulimaliza kundi la ISIS nchini Afghanistan inakaribia mwishoni na ndio maana sasa hivi kundi hili linalipiza kisasi kwa watu wasio na hatia."
Abdul Kabir ameliita kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh kuwa ni Makhawarij na akaongezea kwa kusema, "mashambulizi haya yanafichua sura halisi ya maadui wa Uislamu na Waafghanistan."
Licha ya kauli hiyo iliyotolewa na Naibu waziri mkuu serikali ya muda ya Taliban, mashambulizi ya DAESH yameongezeka baada ya Taliban kuingia madarakani nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021. Kundi hilo sasa linahesabiwa kuwa tishio kuu la kigaidi nchini Afghanistan.../