Saudia yaua Waislamu 15 Yemen katika mwezi wa Ramadhani
(last modified Tue, 21 Jun 2016 14:10:34 GMT )
Jun 21, 2016 14:10 UTC
  • Saudia yaua Waislamu 15 Yemen katika mwezi wa Ramadhani

Watu wasiopungua 15 wameuawa leo katika mashambulizi ya ndege za kivita za Saudi Arabia katika mkoa wa Lahaj huko kusini mwa Yemen.

Mtandao wa al Masirah wa Yemen umeripoti kuwa, ndege za kivita za Saudia pia zimefanya mashambulizi katika mikoa ya Sa'da na Maarab na kuua Waislamu wa Yemen walioko katika mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Vilevile vibaraka wa Saudi Arabia wameshambulia kwa maroketi Eneo la Tisa mjini Sanaa na al Ghawi katika mkoa Taez.

Mauaji hayo yamefanyika baada ya wapiganaji wa Ansarullah kudhibiti eneo la Jabal al Jaalis ambalo lilikuwa ngome kubwa ya vibaraka wa Saudi Arabia wanaoongozwa na Abd Rabbuh Mansur Hadi.

Msemaji wa vibaraka hao wa Saudia, Ali al Muntasir amekiri kwamba, wapiganaji wa harakati ya Ansarullah wamesonga mbele katika maeneo ya kusini mwa Yemen na kwamba wametwaa udhibiti wa eneo la Jabal al Jaalis baada ya mapigano makali ya wiki mbili. Eneo hilo ndilo muhimu zaidi la kijeshi huko Aden kusini mwa Yemen.