Kongamano la kimataifa la Palestina lafanyika Rome Italia
(last modified Wed, 17 May 2023 06:27:51 GMT )
May 17, 2023 06:27 UTC
  • Kongamano la kimataifa la Palestina lafanyika Rome Italia

Kongamano la kimataifa la Palestina katika sheria za kimataifa limefanyika katika ubalozi wa Palestina mjini Rome mji mkuu wa Italia.

Wanasheria na wataalamu mbalimbali wa italia, Palestina na baadhi ya mataifa ya Ulaya wameshiriki katika kongamano hilo lililofanyika jana.

Kuendelea kukiukwa haki za Wapalestina, kukanyagwa haki za binadamu kwa ujumla na jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya wanawake na watoto wa Kipalestina sambamba na hali mbaya ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika kongamano hilo la siku moja mjini Rome.

Waliohutubia kongamano hilo la Palestina katika sheria za kimataifa wamesisitiza kwamba, suala la hali ya haki za binadamu hii leo lina umuhimu mkubwa kwa ajili ya kudhamini amani ikiwa moja ya dharura katika medani ya kimataifa  na kupatiwa haki za kimsingi wananchi wa Palestina.

 

Aidha wazungumzaji katika kongamano hilo wamesema kuanzia mwaka 1967 hadi sasa utawala vamizi wa Israel umewakamata na kuwatia jela zaidi ya Wapalestina 1,200,000 wasio na hatia yoyote.

Yusuf Salman, kiongozi wa jamii ya Wapalestina huko Rome Italia amesema kuwa, kutathmini hali ya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel na kuendelea ukandamizaji dhidi yao unaofanywa na Israel ni miongoni mwa yaliyokuwa malengo ya kongamano hilo.