Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Masjidul-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99874-walowezi_wa_kizayuni_wavamia_tena_masjidul_aqswa
Kwa mara nyingine tena walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wameuvamia tena msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 13, 2023 08:13 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Masjidul-Aqswa

Kwa mara nyingine tena walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wameuvamia tena msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.

Mashuhuda wanasema kuwa, uvamizi wa walowezi hao wenye itikadi kali ulifanyika chini ya ulinzi mkali kutoka kwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa  Israel. 

Hii si mara ya kwanza kwa walowezi wa Kizayuni kuvamia msikiti wa al-Aqswa wakisaidiwa na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno sambamba na njama za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa eneo hilo takatifu.

 

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.