UNAIDS: Ugonjwa hatari wa ukimwi kumalizika duniani ifikapo 2030
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99944-unaids_ugonjwa_hatari_wa_ukimwi_kumalizika_duniani_ifikapo_2030
Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na virusi vya Ukimwi (UNAIDS) limetangaza kuwa, virusi vya HIV na Ukimwi vinaweza kumalizika kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2023 06:47 UTC
  • UNAIDS: Ugonjwa hatari wa ukimwi kumalizika duniani ifikapo 2030

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na virusi vya Ukimwi (UNAIDS) limetangaza kuwa, virusi vya HIV na Ukimwi vinaweza kumalizika kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamo katika ripoti ya UNAIDS ambayo hata hivyo imetahadharisha kwamba,lengo hilo la kuutokomeza ugonjwa wa Ukimwi litafikiwa kama mataifa yataweza kuwa na utashi wa kisiasa na msaada muhimu wa kifedha ili kuushinda kabisa ugonjwa huo.

Ugonjwa huo hatari umeua watu milioni 40.4 tangu kuanza kwa janga hilo mwaka 1981. “Takwimu katika ripoti hii zinaonyesha kuwa njia inayomaliza Ukimwi sio siri, lakini ni chaguo. Ni chaguo la kisiasa na kifedha,” alisema Winnie Byanyima, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na virusi vya Ukimwi (UNAIDS).

 

Ripoti hiyo iliyotolewa na Programu ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na virusi vya Ukimwi (UNAIDS) inaonyesha kuwa, mwaka 2022 watu milioni 39 duniani kote walikuwa wanaishi na virusi vya ukimwi ambapo milioni 1.3 waliambukizwa virusi hivyo na watu 630,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwaka jana (2022) Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi (UNAIDS) lilitangaza kuwa, utafiti upya uliochapishwa kutoka nchini Uholanzi umeonesha kuwepo kwa spishi mpya ya kirusi cha UKWIMI ambacho licha ya kusambaa kwa kasi pia kina madhara zaidi.