Maandamano ya kuunga mkono Palestina yafanyika nchini Marekani
Idadi kubwa ya Wamarekani wameandamana katika miji mbalimbali ya Marekani ambapo wametangaza kuwaunga mkono Wapalestina na kulaani pia jinai za Israel katika kambi ya Jenin huko Palestina.
Maandamano hayo yaliyofanyika pia katika miji mikubwa ya New York na Chicago yalishuhudia waandamanaji wakipiga nara za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.
Maandamano na mkusanyjko mkubwa pia umeshuhudiwa katika mji wa Washington DC ambapo waandamanaji hao wametangaza mfungamano wao na wananchi wa Palestina.
Hivi karibuni jeshi la utawala wa Kizayuni lilitekeleza mashambulizi katika kambi ya wakimbizi huko Jenin kwa ruhusa ya Marekani, mashambulizi ambayo yamesababisha mauaji na uharibifu mkubwa.
Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa na washirika wafadhili Jumapili iliyopita walitembelea kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin, ambapo walishuhudia uharibifu wa kushtua uliofanyika wakati wa uvamizi wa utawala haramu wa Israeli wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) takriban watu 24,000 wanaishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Jenin, ambayo iko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.
Kituo cha afya cha UNRWA hapo kimeharibiwa vibaya kiasi kwamba hakiwezi kutumika tena, na shule zake nne zilipata uharibifu mdogo, shirika hilo limesema.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limewataka wafadhili na washirika kutoa fedha mara moja kwa ajili ya kutekeleza hatua zake za kibinadamu katika kambi hiyo.