Russia yasitisha ushiriki wake kwenye makubaliano ya nafaka ya Bahari Nyekundu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i100010-russia_yasitisha_ushiriki_wake_kwenye_makubaliano_ya_nafaka_ya_bahari_nyekundu
Ikulu ya Kremlin imetangaza kuwa Russia imesitisha ushiriki wake katika makubaliano ya kuruhusu meli ya Ukraine iliyobeba nafaka kuvuka Bahari Nyeusi kuelekea maeneo ya dunia yanayokabiliwa na njaa kwa ajili ya kufikisha bidhaa hiyo, hatua ambayo ni pigo kwa usalama wa chakula duniani, kutokana na ongezeko la bei kufuatia uvamizi wa Moscow dhidi ya Kyiv.
(last modified 2025-11-03T16:45:17+00:00 )
Jul 17, 2023 12:09 UTC
  • Russia yasitisha ushiriki wake kwenye makubaliano ya nafaka ya Bahari Nyekundu

Ikulu ya Kremlin imetangaza kuwa Russia imesitisha ushiriki wake katika makubaliano ya kuruhusu meli ya Ukraine iliyobeba nafaka kuvuka Bahari Nyeusi kuelekea maeneo ya dunia yanayokabiliwa na njaa kwa ajili ya kufikisha bidhaa hiyo, hatua ambayo ni pigo kwa usalama wa chakula duniani, kutokana na ongezeko la bei kufuatia uvamizi wa Moscow dhidi ya Kyiv.

Umoja wa Mataifa na Uturuki zilisimamia mapatano ya kihistoria kati ya Ukraine na Russia mnamo Julai mwaka jana, ambayo yalifuatana na makubaliano mengine tofauti ya kuwezesha usafirishaji wa chakula na mbolea ya Russia ambayo Moscow inasisitiza kuwa hayajatekelezwa.

Mkataba wa Bahari Nyeusi umerefushwa mara kadhaa lakini ulipangwa kumalizika leo Jumatatu jioni.

"Makubaliano ya Bahari Nyeusi yamekoma kuwa halali kisheria leo," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari alasiri ya leo.

Peskov ameongezea kwa kusema: "kwa bahati mbaya, sehemu ya makubaliano haya ya Bahari Nyeusi kuhusiana na Russia haijatekelezwa hadi sasa, kwa hivyo utekelezwaji wake umehitimishwa".

Russia imeifahamisha Uturuki, Ukraine na Umoja wa Mataifa kwamba inapinga kurefusha mkataba huo. Hayo ni kwa mujibu wa Maria Zakharova, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia.

Russia na Ukraine zilipofikia makubaliano ya nafaka kwa usimamizi wa UN na Uturuki

Kusitishwa mkataba huo wa nafaka kumekuja saa chache baada ya Russia kutangaza kuwa Ukraine ilishambulia daraja linalounganisha Russia na rasi ya Crimea.

Ukraine na Russia ni wazalishaji wawili wakubwa wa bidhaa na mazao ya kilimo duniani, na wachangiaji wakuu katika masoko ya ngano, shayiri, mahindi, rapa, mafuta ya rapa, mbegu za alizeti na mafuta ya alizeti. Russia ndio inayoongoza pia katika soko la mbolea.

Makubaliano ya Bahari Nyeusi yalitoa hakikisho kwamba meli hazitashambuliwa zikiingia na kutoka katika bandari za Ukraine. Makubaliano mengine tofauti na hayo yalifikiwa ili kuwezesha usafirishaji wa chakula na mbolea ya Russia, ambavyo navyo pia vina umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya upatikanaji wa chakula duniani.

Gharama kubwa za nafaka zilizochangiwa na athari za vita vya Ukraine, nafaka ambazo zinahitajika kwa ajili ya chakula kikuu katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika zimezidisha changamoto za kiuchumi na kupelekea mamilioni ya watu zaidi kuingia kwenye umaskini au kukabiliwa na uhaba wa chakula.../