Russia yaruhusu kuanzishwa benki za Kiislamu katika baadhi ya maeneo
Bunge la Russia (Duma) limeidhinisha muswada wa sheria inayoruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa benki za Kiislamu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Duma iliidhinisha muswada huo uliowasilishwa kwa mara ya mwisho Bungeni hapo jana, na hivyo kubariki kuanzishwa kwa benki za Kiislamu katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu nchini humo ya Bashkortostan, Chechnya, Daghestan, na Tatarstan.
Sheria hiyo inaruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa benki za Kiislamu katika maeneo hayo kuanzia Septemba Mosi katika hatua ya majaribio, na iwapo mpango huo utafanikiwa ndani ya miaka miwili, basi utapanuliwa na kusambazwa katika maeneo mengine ya nchi hiyo.
Inaarifiwa kuwa, huduma za Kiislamu za kifedha zitatolewa katika fremu ya Mashirika ya Ubia wa Kifedha (FPO) na kuwapa wateja huduma za kifedha zinazofuata sheria za Kiislamu.
Benki za Kiislamu zinafanya kazi chini ya miongozo ya kidini na kimaadili ambapo malipo ya riba ni marufuku. Wazo la kuanzisha benki za Kiislamu nchini Russia limejadiliwa kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mashirika hayo yanaweza kukusanya fedha kutoka kwa watu binafsi na vyombo vya kisheria na kuwekeza katika miradi kulingana na kanuni za sheria za Kiislamu kwa misingi ya ushirikiano.
Wachumi wanasema Russia imeidhinisha benki hizo kama sehemu ya jitihada za kuvutia wawekezaji kutoka nchi za Kiislamu ili kukabiliana na vikwazo ambavyo benki za nchi hiyo zimewekewa na Wamagharibi.