Jul 29, 2023 04:17 UTC
  • Upinzani Sweden wamtaka mbunge aliyemtusi Mtume (saw) kujiuzulu

Upinzani nchini Sweden umemtaka mkuu wa Kamati ya Haki Bungeni na mwanachama wa chama cha Democrats kujiuzulu, baada ya kuchapisha maandishi ya kumkashifu Mtume Muhammad (saw) kupitia mitandao ya kijamii, huku Waziri wa Sheria wa Sweden akikiri kwamba, matukio ya kuchomwa moto Qur'ani Tukufu yameathiri vibaya sura ya nchi yake.

Mwanasiasa mwenye misimamo ya kuchupa mipaka wa mrengo wa kulia wa Sweden, Richard Yumshov, ambaye ni mkuu wa Kamati ya Haki Bungeni na mwanachama wa chama cha Demokrasia cha nchi hiyo amechapisha maandishi ambamo amemtusi Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw), akipinga wito uliotolewa na Waislamu wa Sweden wa kuwepo mazungumzo kwa lengo la kukomesha vitendo vya kichochezi vya kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu.

Baada ya hatua hiyo, Mwenyekiti wa chama kikubwa zaidi cha upinzani cha Swedish Social Democrats, Magdalena Andersson, amemtaka Yumshov ajiuzulu mara moja nafasi ya urais wa Kamati ya Bunge.

Vilevile msemaji wa mambo ya nje wa chama cha Social Democrats, Morgan Johansson, amesema katika taarifa yake kwenye gazeti la Aftonbladet, kwamba Yumshov hawezi kubaki katika nafasi yake, na kwamba lazima ajiuzulu.

Awali Waziri wa Sheria wa Sweden, Gunnar Strömmer, alitangaza kuwa matukio ya kuchomwa moto nakala za Qur’ani yamesababisha hali mbaya ya usalama katika nchi yake, na kuathiri vibaya taswira ya nchi hiyo nje ya nchi.

Gunnar Strömmer

Strömmer amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba, kuchomwa moto Qur'ani Tukufu na maandamano yanayofanyika katika pembe mbalimbali za dunia kupinga vitendo hivyo yameidhihirisha Sweden kama nchi yenye chuki dhidi ya Waislamu.

Itakumbukwa kuwa, Jumanne iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kulaani aina zote za kuvunjiwa heshima vitabu vitakatifu likitambua vitendo vya aina hiyo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinishwa baada ya Qur'ani Tukufu kuvunjiwa heshima katika  nchi za Sweden na Denmark, suala ambalo limeibua hasira na na malalamiko makali ya mataifa ya Kiislamu kote duniani. 

Tarehe 12 mwezi huu wa Julai pia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio lililopendekezwa na nchi za Kiislamu la kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kumtaka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kufanya uchunguzi kuhusu jambo hilo pamoja na kutoa ripoti kuhusu uchunguzi huo.

Tags