Matukio ya ufyatuaji risasi yaongezeka US; 25,000 wameuawa 2023
https://parstoday.ir/sw/news/world-i100576-matukio_ya_ufyatuaji_risasi_yaongezeka_us_25_000_wameuawa_2023
Taasisi ya kukusanya data zinazohusiana na matukio ya ufyatulianaji risasi nchini Marekani imetangaza kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2023 hadi sasa, zaidi ya watu 25,000 wameuawa kwa silaha za moto kote nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2023 22:49 UTC
  • Matukio ya ufyatuaji risasi yaongezeka US; 25,000 wameuawa 2023

Taasisi ya kukusanya data zinazohusiana na matukio ya ufyatulianaji risasi nchini Marekani imetangaza kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2023 hadi sasa, zaidi ya watu 25,000 wameuawa kwa silaha za moto kote nchini humo.

Ripoti ya taasisi ya "Gun Violence Archive"  imesema idadi hiyo inaashiria wastani wa vifo 118 kwa siku; huku ikionya kuhusu ongezeko la kuogofya la matukio ya ufyatuaji risasi kiholela nchini humo.

Ripoti hiyo imesema, kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, kumekuwapo na matukio 419 ya ufyatulianaji wa risasi nchini Marekani. Mbali na watu 25,000 kuuawa kwa mtutu wa bunduki mpaka sasa, wengine zaidi ya 22,000 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa Gun Violence Archive, katika watu 118 wanaouawa kila siku kwa kupigwa risasi nchini Marekani, mmoja ni mtoto mwenye chini ya miaka 11, na wanne ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17.

Kiwango cha mauaji ya silaha za moto katika nchi hiyo ni kikubwa zaidi kuliko nchi nyingine yoyote duniani; na takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha sasa cha mauaji ya watu kwa bunduki nchini Marekani ndicho cha juu zaidi ikilinganishwa na miaka 30 iliyopita. 

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Uswisi linalohusika na masuala ya umiliki wa bunduki la "Small Arms Survey", Marekani ndiyo nchi pekee duniani ambako idadi ya silaha ni kubwa kuliko idadi ya watu.