Papa Francis atoa mwito wa kushughuliwa hali ya wahamiaji barani Ulaya
Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ametoa mwito wa kushughuliwa hali ya wahamiaji barani Ulaya.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema hayo na kubainisha kwamba, vifo vya wahamiaji katika Bahari ya Mediterania ni kidonda kilicho wazi na kwamba, kidonda hiki kinapaswa kushughuliwa kwa bandeji na dawa na viongozi wa kisiasa wa Ulaya.
Akionyesha kusikitishwa na vifo vya mara kwa mara vya wahamiaji katika maji ya Bahari ya Mediterania, Papa Francis amesema inasikitisha kwamba, tangu kuanza mwaka huu karibu watu 2000 wakiwemo wanawake na watoto wamekufa maji wakiwa njiani kuelekea Ulaya.

Ikumbukwe kuwa, mwaka jana (2022), wahamiaji 24,684 waliokolewa na kurudishwa Libya, wahamiaji 525 walikufa na wengine 848 walipotea kwenye pwani ya Libya.
Libya imekuwa kituo kikuu cha wahamiaji haramu wanaoelekea barani Ulaya kutokana na ukosefu wa usalama, machafuko na kukosekana serikali kuu yenye nguvu nchini humo tangu ulipoangushwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Wahamiaji wengi wanatokea nchi za Afrika za chini ya Jangwa la Sahara na wengi wao huwa wanakufa maji kutokana na kutumia vyombo dhaifu sana kama mitumbwi ya plasitiki kuvuka mikondo mikali ya bahari kubwa ya Mediterania.
Ripoti zinaonyesha kuwa, wahamiaji 400 walifariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu ya awali ya mwaka huu katika bahari ya Mediterania.