Aug 16, 2023 02:50 UTC
  • Onyo kuhusu ongezeko kubwa la itikadi kali za kisiasa nchini Marekani

Wakati kesi ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ikiendelea sambamba na kuandaliwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo wa mwaka 2024, wataalamu wametahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la misimamo mikali ya kisiasa miongoni mwa Wamarekani.

Vitisho dhidi ya maafisa wa serikali ya Marekani vimekuwa vikiongezeka mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni na vimeibua changamoto mpya kwa utekelezaji wa sheria, haki za kiraia na kile kinachodaiwa kuwa ni demokrasia ya Marekani.

Kulingana na jarida la Politico la Marekani, moja ya vitisho vya hivi karibuni zaidi ni makabiliano ya mzee wa miaka 74 katika jimbo la Utah na maafisa wa Idara ya Upelelezi ya Shirikisho la Marekani (FBI). Makabiliano hayo  hatimaye yalisababisha kifo cha mzee huyo. Inasemekana mzee huyo alikuwa ametishia kwenye mtandao wa kijamii kuwa angemuua Rais Joe Biden wa Marekani .

Kwa hiyo, wataalamu wameonya kuhusu kushadidi misimamo mikali ya Wamarekani  sambamba na ongezeko la ghasia zenye muelekeo wa kisiasa.

Wiki iliyopita, mtu wa miaka 52 kutoka jimbo la Texas alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu jela kwa kutishia kuwaua wafanyikazi wa uchaguzi katika jimbo la Arizona. Siku nne kabla ya tukio hilo, waendesha mashtaka walitangaza kukamatwa kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 56 kutoka jimbo la Michigan ambaye alidanganya kuhusu kununua bunduki kwa ajili ya mtoto wake mwenye ulemavu wa akili, lakini alikusudia kuitumia dhidi ya Biden na gavana wa chama cha Democrat katika jimbo hilo. Kitengo cha Polisi katika Bunge la Marekani, Congress, kilitangaza katika ripoti yake mwaka jana kwamba idadi ya vitisho dhidi ya wabunge imeongezeka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.

Magenge ya wafuasi wenye misimamo mikali wa Trump wakiwa ndani ya jengo la Congress, Capitol, kujaribu kuvuruga matangazo ya uchaguzi wa rais

Kuna mgawanyiko mkubwa wa kijamii kutokana na kuwepo kwa tofauti nyingi kati ya vyama viwili vikuu vya Marekani, yaani chama cha upinzani cha Republican na chama tawala cha Democratic, hasa kati ya Donald Trump na Joe Biden, marais wa zamani na wa sasa wa Marekani. Magwanyiko huu mkubwa unazidi kuongezeka kote Marekani .

Aidha  mitazamo inayokinzana mara kwa mara kuhusu masuala ya sera za ndani na nje ya Marekani, ambayo imezua taharuki katika maamuzi, sasa inadhihirika kikamilifu.

Jambo hilo limesababisha ongezeko kubwa la misimamo mikali ya kisiasa na kuibuka kwa vitisho visivyo na mfano wake dhidi ya mamlaka na taasisi za shirikisho na serikali nchini Marekani. Kuongezeka migawanyiko ya ndani, haswa kati ya watu ambao hawajaridhika na serikali za majimbo na serikali ya kitaifa kumekuwa na nafasi kubwa katika kushadidisha tishio jipya la usalama, yaani, ongezeko kubwa la vitisho na vitendo vya kigaidi vinavyotekelezwa na watu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia.

Alejandro Mayorkas, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani anasema: Misimamo mikali ya majumbani ni moja ya vitisho vikubwa vinavyohusiana na ugaidi nchini Marekani

Wataalamu wa masuala ya Marekani wanasema moja ya sababu kuu za hali ya sasa ni madai yasiyothibitishwa ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye ameikosoa vikali FBI na pia kutilia shaka itibari ya Idara ya Mahakama ambayo imekuwa ikilaumiwa na  rais huyo wa zamani tangu kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020.

Sisitizo la Trump kuwa kulikuwa na wizi wa kura mbao ulipelekea Biden kushinda uchaguzi uliopita wa rais ni jambo ambalo limepelekea kuongezeka vitisho dhidi ya wafanyikazi wa uchaguzi kiasi kwamba mtu mmoja kati ya sita wanaofanya kazi katika idara ya  uchaguzi wameripoti kupokea vitisho.

Wakati huo huo, inasemekana kuwa wasimamizi wengi wenye uzoefu wa kuendesha zoezi la uchaguzi wameacha kazi zao au wanafikiria kuiacha.

Wanamgambo wafuasi wa Trump

Michael German, afisa wa zamani wa FBI, anasema:  Ushahidi unaonyesha kuwa Trump na wanachama wengi wa chama cha upinzani cha Republican, kimsingi wameanza kukuza magenge ya vurugu na kuhimiza watu wa kawaida kujihusisha na vitendo vya ghasia.”

Wataalamu wameonya kwamba vitisho hivyo haviishiii tu katika maneno makali kwani vimeanza kugeuka na kuwa msingi wa ghasia na machafuko ya kisiasa. Weledi wa mambo wanasema kukithiri matamshi hayo, hasa wakati wa kukaribia uchaguzi wa 2024 na huku kesi ya Trump ikiwa inaaza, kunaweza kuongeza hatari ya vurugu na ghasia za wenywe kwa wenyewe nchini Marekani.

Javed Ali, afisa mkuu wa zamani wa FBI wa kukabiliana na ugaidi, anasema: "Wasiwasi mkubwa ni washambuliaji wanaotekeleza hujuma kwa kutegemea maamuzi. Mshambuliaji kama huyo si kama wale walioratibiwa na kutetekeleza shambulio dhidi ya jengo la Congress katika ghasia kubwa za Januari 6, 2021. Mashambulizi ya kujituma  ni hatari zaidi kwa sababu mtu anaweza kutekeleza hujuma haraka sana na bila taarifa ya awali.”

Tags