Wasiwasi wa Waislamu Ujerumani wa kuongezeka hujuma dhidi ya misikiti
(last modified Thu, 17 Aug 2023 07:24:16 GMT )
Aug 17, 2023 07:24 UTC
  • Wasiwasi wa Waislamu Ujerumani wa kuongezeka hujuma dhidi ya misikiti

Mamilioni ya Waislamu nchini Ujerumani wana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na hujuma na mashambulio dhidi ya misikiti nchini humo.

Kemal Ergon, mkuu wa kundi la Waislamu nchini Ujerumani anasema kuwa, misikiti zaidi imepokea barua za vitisho katika wiki za hivi karibuni zilizotiwa saini na jina bandia la Wanazi mamboleo "NSU 2.0".

Ameongeza kuwa, inasikitisha kuwa katika matukio mengi ya moto ya misikiti, ambayo yanaweza kuua watu wengi, wahusika hawatambuliki wala kukamatwa.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu (2023), kulifanyika mashambulizi 124 dhidi ya Waislamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya maneno na ya kimwili, barua za vitisho na kuchomwa moto misikiti nchini Ujerumani.

Takwimu za karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, polisi wa Ujerumani walirekodi angalau uhalifu 610 wa chuki dhidi ya Uislamu kote nchini humo mwaka jana (2022).

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu

Takriban misikiti 62 ilishambuliwa nchini Ujerumani kati ya Januari na Disemba mwaka jana na watu wapatao 39 walijeruhiwa kutokana na hujuma na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu.

Ujerumani ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 84 na Waislamu karibu milioni 5.3, inahesabiwa kuwa nchi ya pili kwa idadi kubwa ya Waislamu katika Ulaya Magharibi baada ya Ufaransa.

Katika miaka ya hivi karibuni, Ujerumani imeshuhudia ongezeko la ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu, ikichochewa na propaganda za Wanazi mamboleo na vikundi vya kufurutu ada vya mrengo wa kulia vya AfD, ambavyo vinatumia vibaya mgogoro wa wahajiri  na vinajaribu kuwatia hofu wahamiaji.