Aug 25, 2023 08:04 UTC
  • Njama za Uingereza za kuzuia uchunguzi kuhusu jinai za wanajeshi wake duniani

Kwa mujibu wa televisheni ya Sky News, serikali ya Uingereza inatumia vizingizio mbalimbali vya kuzuia uchunguzi kuhusu jinai za wanajeshi wake katika nchi nyingi duniani vikiwemo visingizio vya kiusalama.

Hii ni katika hali ambayo ripoti zote zilizosambazwa na mashirika tofauti ya habari daima zinaonesha kuwa wanajeshi na Uingereza na Ujerumani wamehusika katika jinai dhidi ya binadamu ikiwa ni pamoja na huko Afghanistan kwa mgongo wa jeshi la nchi za Magharibi NATO. Hata uchunguzi wa shirika moja la haki za binadamu la Uingereza unaonesha kuwa, wanajeshi wa kikosi maalumu cha Uingereza nchini Afghanistan waliua raia wasiopungua 80 katika kipindi cha baina ya mwaka 2010 na 2014. Hiyo ni sehemu ndogo tu ya jinai nyingi za wanajeshi wa Uingereza duniani. Shirika hilo la haki za binadamu lililazimika kuchunga sheria zote za Uingereza ndipo lilipoweza kufichua angalau sehemu hiyo ndigo ya jinai za wanajeshi wa nchi hiyo. Abbas Fayadh, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anasema:

"Wanajeshi wa Uingereza ambao ni sehemu ya wanajeshi walioivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan katika kipindi cha miaka 20, daima walikuwa wanawadhalilisha na kufanya jinai dhidi ya wananchi wa nchi hiyo. Vitendo vyao ni sawa na unyanyasaji wanaofanyiwa watu weusi nchini Marekani kiasi kwamba wanajeshi vamizi wa Uingereza walijipa haki ya kufanya unyama wowote wanaotaka dhidi ya wananchi wa Afghanistan."

Wanajeshi vamizi wa UIngereza

 

Ripoti nyingi zinaonesha kuwa, wanajeshi wa Uingereza baadhi ya wakati walikuwa wanafanya mauaji ya raia kwa ajili ya kujifurahisha tu. Wanajeshi wa Uingereza wanahusishwa pia na mateso na mauaji ya wafungwa katika jela mbalimbali zisizo rasmi ikiwa ni pamoja na huko Afghanistan na Iraq. Hamid Karzai, rais wa zamani wa Afghanistan anasema, vitendo vya kikatili vya wavamizi wa nchi yake hasa Waingereza na Wamarekani vilikuwa vikubwa kiasi kwamba walikuwa wanavamia nyumba za watu nyakati za usiku na kuwateka nyara wananchi bila ya hofu yoyote.

Ijapokuwa hakuna ripoti huru na uchunguzi wa kina wa jinai za wanajeshi wa Uingereza dhidi ya raia lakini jinai zao ni kubwa kiasi kwamba hata hiyo sehemu ndogo ambayo hutokezea baadhi ya wakati ikafichuka; ni ya kutisha. Kabla ya kufichuliwa jinai za Uingereza huko Afghanistan hivi karibuni, serikali ya London iliamua kujitoa kimasomaso kwa madai ya kufanya uchunguzi kuhusu jinai hizo. Awali viongozi wa Uingereza walidai kuwa watafanya uchunguzi huru na wazi lakini baadaye wameamua kufanya kwa siri na kificho uchunguzi kuhusu uhalisia wa mambo kiasi kwamba wachambuzi wengi hawana imani hata kidogo na madai hayo ya viongozi wa London.  Asadullah Zaeri, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema:

"Wananchi wa Afghanistan walipitisha kipindi kigumu sana cha kukaliwa kwa mabavu nchi yao na madola vamizi ikiwemo Uingereza. Wanajeshi wa Uingereza walitumia fursa yoyote waliyopata kufanya mauaji na kuwanyanyasa wananchi wa Afghanistan. Pembeni mwa mauaji makubwa yaliyofanywa na  wanajeshi vamizi wa UIngereza dhidi ya raia, wanajeshi hao walitumia mabomu yaliyopigwa marufuku dhidi ya watu wa kawaida na kusababisha kuzuka magonjwa ya kila namna ya kiakili, ya ngozi na ya mwilini kati ya wananchi wa Afghanistan."

Wanajeshi vamizi nchini Afghanistan

 

Ijapokuwa wizara ya ulinzi ya serikali ya kifalme ya Uingereza inatumia visingizio kama vya kiusalama na kuingilia masuala ya watu binafsi kujaribu kuzuia kufanyika uchunguzi zaidi dhidi ya jinai za wanajeshi wa Uingereza duniani, lakini ni wazi kwamba hawawezi kuficha ukweli milele.

Gazeti la The Times la Uingereza hivi karibuni lilifichua kuwa, kabla ya wachunguzi kutembelea vituo cha vikosi maalumu vya Uingereza kama sehemu ya kufanya uchunguzi kuhusu jinai za wanajeshi hao ulimwenguni, makamanda wa jeshi la Uingereza walifuta na kuteketeza mafaili yote ya jinai hizo. Hali hiyo wameifanya pia katika nchi nyinginezo kama Australia na katika nchi za Afrika zilizokoloniwa na mkoloni huko kizee wa barani Ulaya yaani Uingereza.

Suala la jinai za kivita za wanajeshi wa Uingereza ziko wazi mbele ya macho ya walimwengu na kama tulivyosema, jinai hizo ni kubwa kiasi kwamba haiwezekani kuzificha na hata kama itachukua muda kufichuliwa, lakini hatimaye dunia itaelewa tu jinai za wanajeshi vamizi wa dola la kikoloni la ufalme wa Uingereza.

Tags