Hujuma dhidi ya Uislamu zaongezeka Uingereza baada ya Brexit
Waislamu wa Uingereza wanakabiliwa na wimbi kubwa la hujuma zinazotokana na chuki baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni ya kujiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya (Brexit).
Toleo la leo la gazeti la Independent limenukuu kundi la Tell Mama ambalo linasajili na kupima matukio ya hujuma dhidi ya Waislamu nchini Uingereza kwamba mashambulizi yanayotokana na propaganda chafu dhidi ya Uislamu yameongezeka kwa asilimia 326 katika mwaka uliopita na sasa yameshika kasi zaidi.
Ripoti ya Tell Mama imesema kuwa, wanawake wa Kiislamu wanaotumia vazi la hijabu nchini Uingereza wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwa kadiri kwamba, wanashindwa kufanya kazi zao za kila siku kwa kuchelea mashambulizi. Ripoti hiyo inaonesha kuwa, asilimia 61 ya wahanga wa mashambulizi hayo ni wanawake wenye vazi la hijabu.
Ripoti ya Tell Mama pia imeashiria kwamba, idadi kubwa ya wanaotekeleza mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini Uingereza wana umri wa kati miaka 13 na 18 na kusema kuwa, fikra za misimamo ya kuchupa mipaka zimeongeza kati ya vijana wa Uingereza.
Waziri wa zamani wa kazi wa Uingereza Shahid Malik ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tell Mama, ameitaka serikali ya nchi hiyo kutupilia mbali fikra zisizo sahihi na kutambua kuwa, kujiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya kumeifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi kwa jamii za waliowachache nchini humo.