Waziri wa Russia: BRICS itaanzisha mfumo mbadala wa SWIFT
https://parstoday.ir/sw/news/world-i102858-waziri_wa_russia_brics_itaanzisha_mfumo_mbadala_wa_swift
Waziri wa Fedha wa Russia amedokeza kuwa, nchi wanachama wa kundi la BRICS zinajiandaa kuanzisha mfumo wa mawasiliano ya kibenki kama mbadala wa ule wa SWIFT wa Wamagharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2023 01:08 UTC
  • Waziri wa Russia: BRICS itaanzisha mfumo mbadala wa SWIFT

Waziri wa Fedha wa Russia amedokeza kuwa, nchi wanachama wa kundi la BRICS zinajiandaa kuanzisha mfumo wa mawasiliano ya kibenki kama mbadala wa ule wa SWIFT wa Wamagharibi.

Anton Siluanov amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la TASS na kueleza kuwa, suala hilo la kuanzisha mfumo mbadala wa SWIFT litajadiliwa na nchi wanachama wa BIRCS katika mkutano wa jumuiya hiyo ya kiuchumi mwaka ujao.

Siluanov amesema hayo katika mkutano wa Jukwaa la Fedha la Moscow na kuongeza kuwa, nchi kadhaa wanachama wa kundi la BRICS tayari zimeanzisha mifumo binafsi ya malipo.

SWIFT ambayo ina maana ya Society for Worldwide Interbank Financial Telecommunication (SWIFT), yaani Jumuiya ya kimataifa ya Mawasiliano ya Kibenki inaziunganisha benki na taasisi nyingine za fedha kote duniani ili kubadilishana taarifa za masuala ya fedha kati ya taasisi hizo kwa njia ya amani.

Japokuwa mtandao wa SWIFT unadai kwamba, haupendelei upande wowote katika masuala ya kisiasa lakini hivi sasa imebainika wazi kuwa, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinautumia mfumo huo kama wenzo wa kufanikisha malengo ya siasa zao za nje na za kifedha.

Waziri wa Fedha wa Russia ameeleza bayana kuwa, nchi wanachama wa kundi la BRICS zinachukua hatua za dharura za kuanzisha mfumo wa mawasiliano ya kibenki kama mbadala wa ule wa SWIFT.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Russis amesisitiza kuwa, "Jumuiya ya kiuchumi ya BRICS inatafuta mifumo mibadala ya kimataifa ya malipo, kwa kutumia mikakati ambayo itasaidia kuimarisha biashara miongoni mwa nchi wanachama."