Oct 02, 2023 15:13 UTC
  • OIC yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani, yaitaka Sweden kuzuia vitendo hivyo viovu

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa wito mpya kwa serikali ya Sweden ikiitaka kuchukua hatua za haraka dhidi ya watu wanaochoma moto nakala za Qur'ani Tukufu, kwa sababu kitendo hicho ni chuki ya kidini.

Taarifa iliyotolewa leo na Sekretarieti Kuu ya Jumuiya ya Kiislamu yenye makao yake makuu mjini Jeddah, magharibi mwa Saudi Arabia, imelaani kwa "maneno makali" kitendo cha uchochezi na cha kukaririwa cha kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu siku ya Jumamosi iliyopita katika mji wa Malmö, nchini Sweden, licha ya wito wa mara kwa mara uliotolewa kwa serikali ya Uswidi kuzuia kukaririwa vitendo kama hivyo.

Katibu Mkuu wa OIC, Hissein Brahim Taha, amekariri wito wa jumuiya hiyo "kwa serikali ya Sweden akiitaka kuchukua hatua za haraka dhidi ya vitendo hivyo vya uchochezi ambavyo ni kielelezo cha chuki ya kidini na vinatambuliwa kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa."

Hissein Brahim Taha

Mkazi wa Sweden, Salwan Momika Jumamosi iliyopita alikariri kitendo kiovu na cha kishenzi cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu mjini Malmö kwa kibali rasmi cha polisi ya nchi hiyo.

Katika miezi ya karibuni, Momika amechoma moto Msahafu mara kadhaa na kuibua hisia kali duniani za kukemewa, kupingwa na kulaaniwa kitendo chake hicho. Aliwahi kufanya kitendo hicho kiovu kwa kibali rasmi cha Polisi ya Sweden tena mbele msikiti mkuu wa Stockholm hata katika moja ya Sikukuu kubwa ya Waislamu ya Idul-Adh'ha iliyosadifiana na tarehe 28 Juni mwaka huu.

Serikali na viongozi wa Sweden ambao wamedai mara kadhaa kuwa watachunguza vitendo hivyo kisheria na kisiasa wanaendelea kuunga mkono jinai hizo dhidi ya Uislamu na kuzidi kuchochea hisia za Waislamu duniani.

Tags