Putin: Hakuna adui atakayesalimika katika shambulizi la kisasi la nyuklia
Rais Vladimir Putin wa Russia ametahadharisha kuwa, hakuna adui atakayesalimika iwapo Russia itatekeleza shambulizi la kulipiza kisasi kwa kutumia silaha za nyuklia.
Putin alitoa indhari hiyo jana Alkhamisi katika hotuba yake mbele ya Jukwaa la Midahalo ya Kimataifa la Valdai na kusisitiza kuwa, amani ya kudumu itapatikana iwapo kila mmoja atahisi kuwa ana usalama na maoni yake yanaheshimiwa.
Amesema Russia haikuanzisha mgogoro wa Ukraine, na inachojaribu kufanya ni kuzima mzozo huo. "Vita vilianzishwa na utawala wa Ukraine kwa msaada wa Magharibi, na sasa vipo katika mwaka wake wa 10. Operesheni yetu ya kijeshi inakusudia kusimamisha vita hivyo," amesisitiza Putin.
Rais Vladimir Putin wa Russia ameonya kuwa, hakutakuwa na mshindi katika vita vya nyuklia na kwamba mzozo kama huo haupaswi kuanzishwa.
Kuongezeka mivutano kati ya Russia na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO baada ya vita vya Ukraine, kumezidisha uwezekano wa kutumiwa silaha za nyuklia katika mizozo inayoweza kutokea katika siku za usoni. Hivi karibuni, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alionya kuhusu dunia kuingia katika mashindano mapya ya silaha za nyuklia ambayo yanaweza kueneza maafa duniani kote.
 
Rais Putin amebainisha kuwa, mgogoro wa Ukraine hauna mfungamano wowote na vita vya kupigania ardhi, kwani Russia ndiyo nchi yenye ardhi kubwa zaidi duniani.
Amesema, "hakuna mgogoro wa kupigania ardhi, au hata kuleta mlingano wa nguvu za kijiopolitiki katika eneo, bali ni kuhusu suala muhimu zaidi...tunazungumzia misingi ya Nidhamu Mpya ya Dunia."
 
							 
						 
						