EU: Israel inakanyaga sheria za kimataifa kwa kuiwekea mzingiro Gaza
(last modified Wed, 11 Oct 2023 12:08:25 GMT )
Oct 11, 2023 12:08 UTC
  • EU: Israel inakanyaga sheria za kimataifa kwa kuiwekea mzingiro Gaza

Umoja wa Ulaya umesema kuwa utawala wa Israel umekiuka sheria za kimataifa kwa kuuweka Ukanda wa Gaza chini ya mzingiro.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya baada ya kufanya mkutano wa dharura jana jioni wamekiri kuwa, Israel imekanyaga sheria za kimataifa kwa kuweka mzingiro kamili dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya amesema: Umoja wa Mataifa umeshatangaza kuwa, kuikatia maji, umeme na chakula halaiki ya watu ambao ni raia ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Borrell ameongeza kuwa, huenda mgogoro wa sasa ukaleta mwamko, na kuipelekea jamii ya kimataifa kuangalia upya matatizo ya Wapalestina, Palestina na Israel.

EU imetoa tamko hilo baada ya utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel kutangaza juzi Jumatatu kuwa, unaliwekea mzingiro wa marufuku ya kila kitu eneo la Ukanda wa Gaza kwa kusitisha ufikishaji wa chakula na maji na pamoja na huduma ya umeme, na kuzua hofu ya kuwa mbaya zaidi hali ya kusikitisha na kukatisha tamaa ya kibinadamu inayoshuhudiwa katika eneo hilo.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya

Hii ni katika hali ambayo, jana Jumanne, Volker Turk, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema, mzingiro wa kila kitu ambao Israel imeamua kuuwekea Ukanda wa Gaza, na kuwanyima raia bidhaa muhimu kwa ajili ya maisha, umepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa.

Taarifa ya Turk imesisitiza kuwa, kuweka mzingiro unaohatarisha maisha ya raia kwa kuwanyima bidhaa muhimu kwa maisha yao ni marufuku chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.

Tags