Russia: Marekani haitakuwa tena mhimili mkuu katika "utaratibu mpya wa dunia"
Russia imekosoa matamshi ya rais Joe Biden wa Marekani kwamba Washington lazima iwe ndiyo nguvu inayoongoza katika "utaratibu mpya wa dunia", ikisema maono kama hayo ya "Marekani kuwa mhimili mkuu" yamepitwa na wakati.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi kwamba ingawa anakubaliana na wazo la hitajio la kuwepo "utaratibu mpya wa dunia", lakini haamini kama Marekani ndiyo inapasa kushika usukani wa suala hilo.
Peskov amesema mfumo wowote mpya unapaswa uwe "huru na ukusanyaji wa taratibu zote za uendeshaji masuala ya ulimwengu kwenye mikono ya serikali moja".
Msemaji wa serikali ya Russia ametangaza msimamo huo kujibu hotuba ya Rais wa Marekani Joe Biden aliyoitoa siku ya Ijumaa ambapo alizungumzia ushiriki wa Marekani katika migogoro ya nje kuanzia Ukraine na Taiwan hadi wa Israel.
Katika hotuba yake hiyo Biden alisema "utaratibu wa dunia" wa nusu karne iliyopita "umeishiwa nguvu" na Marekani inahitaji "kuunganisha ulimwengu" katika mpangilio mpya wa kuleta amani.
Peskov amejibu kauli hiyo ya rais wa Marekani kwa kusema: "katika sehemu hii hatukubaliani kwa sababu Marekani, ... bila kujali ni utaratibu gani wa dunia wanaozungumzia, wanamaanisha utaratibu wa ulimwengu unaozingatia Marekani, yaani, ulimwengu unaozunguka mhimili wa Marekani. Haitakuwa hivyo tena.”
Mkwaruzano huo wa maneno baina ya Moscow na Washington unaakisi mvutano na mtafaruku mkubwa uliopo kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani, ambayo yanapingana vikali katika kadhia ya vita kati ya Russia na Ukraine na vilevile ushirikiano unaoshamiri kati ya Moscow na mataifa ambaya Marekani ina uadui nayo mkubwa, yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Korea Kaskazini.../