Nov 05, 2023 13:41 UTC
  • Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yafanyika Ujerumani, Italia

Maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin kushiriki maandamano ya kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, huku idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa katika mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza ikipindukia 10,000.

Wananchi hao wa Ujerumani walioshiriki maandamano hayo wameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dharura za kusimamisha mashambulizi hayo ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yaliyokuwa na jumbe za kuitaka Israel isitishe mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina wasio na hatia.

Aidha baadhi ya mabango hayo yalikuwa na jumbe za kuunga mkono ukombozi wa taifa huru la Palestina. Hali kadhalika waandamanaji hao wamesema hatua ya Marekani kwa kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu inashiriki katika mauaji ya halaiki ya Wazayuni huko Gaza.

Wakati huo huo, wananchi wa Italia hapo jana walimiminika katika barabara za mji mkuu Rome kushiriki maandamano ya kutangaza mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina, sanjari na kulaani mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Waandamanaji hao mjini Rome wamesema utawala katili na usiojali thamani za kiutu wa Israel umekiuka sheria zote za kimataifa, ambapo unashambulia kwa mabomu hospitali, shule na makazi ya raia wa kawaida.

Wameutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati na kukomesha jinai zinazofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza, huku wakiitaka serikali ya Paris isimamishe misaada yake mara moja kwa utawala wa Kizayuni.

Maandamano sawa na hayo dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza yameendelea kufanyika katika nchi mbali mbali za Magharibi, na tayari yameshafanyika katika nchi kama Ufaransa, Denmark, Marekani na Uingereza.

Tags